Shaka aeleza mwenendo wa kampeni umetoa mwangaza kushinda kwa kishindo
Na MWANDISHI WETU
WAKATI wananchi katika Jimbo la Amani, Zanzibar na kata saba zilizopo kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, leo wakipiga kura kuchagua mbunge na madiwani, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimeridhishwa na mwenendo wa kampeni na kinatarajia kupata ushindi.
Taarifa iliyotolewa na CCM na kutiwa saini na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ilisema tathimini kuhusu kampeni iliyofanywa na Chama imeonyesha zilikwenda vizuri.
"CCM imeridhishwa kwa kiasi kikubwa na mwenendo wa kampeni zake za uchaguzi mdogo zilizozinduliwa tarehe 1, Desemba, 2022 na zinazo kamilika leo 16, Desemba, 2022. (jana).
"Kampeni hizi mpaka sasa zimefanywa kwa weledi na umahiri mkubwa. Mwenendo wake umekuwa mzuri sana na CCM ina uhakika wa kushinda kwa kishindo cha zaidi ya asilimia 90," alisema Shaka katika taarifa hiyo kwa umma.
Alisema CCM ikiongozwa na wagombea wake mahiri imefanya kampeni nzuri kupitia mikutano ya hadhara, kukutana na makundi ya wazee, vijana na wanawake na kunadi sera zake kama zilivyoainishwa katika Ilani yake ya Uchaguzi ya 2020 - 2025.
UBUNGE AMANI
Kwa mujibu wa Shaka, kuhusu kiti cha ubunge Jimbo la Amani Zanzibar, CCM ilimteua Abdul Yussuf Maalim kupeperusha bendera yake na kwamba Chama kinaamini atapata ushindi mkubwa kwa kuwa anakubalika.
Aidha, Shaka alisema pia Chama kinashiriki uchaguzi katika kata saba kati ya 12 kwa upande wa Tanzania Bara ambazo ni Majohe (Dar es Salaam), Mwamalili (Shinyanga) Njombe (Njombe), Vibaoni, Mnyanjani (Tanga), Mndubwe (Mtwara) na Dunda (Pwani).
Mbali na hizo, alisema kaata tano kati ya 12 tayari CCM imeshinda kwa kupita bila kupingwa ambazo ni Dabalo (Dodoma), Ibanda (Mbeya), Misugusugu (Pwani), Kalumbeleza (Rukwa) na lukozi (Tanga).
TUTAKUBALI MATOKEO
Shaka alieleza kuwa Hata hivyo Chama kipo tayari kupokea matokeo yoyote katika uchaguzi huo kwa kuwa CCM ndicho Chama kilichobeba na kusimamia demokrasia ya kweli ya vyama vingi nchini.
Uchaguzi mdogo katika jimbo la Amani unafanyika leo kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehemu Mussa Hassan.
No comments:
Post a Comment