Habari za Punde

Waandishi wa Vitabu na Riwaya mbalimbali Nchini, Kuitumia Fasihi katika Kuhifadhi Mila, Desturi na Utamaduni wa Nchi.

Na Maulid Yussuf WMJJWW  Zanzibar 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar  Mhe Riziki Pembe Juma amewataka waandishi wa vitabu na riwaya mbalimbali nchini, kuitumia fasihi katika kuhifadhi mila, desturi na utamaduni wa nchi.

Mhe. Riziki ameyasema hayo leo, wakati alipozindua Riwaya ya Fanani, iliyotungwa na ndugu Zainab Alwi Baharoon, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Studio ya muziki Rahaleo Mjini Unguja.

Amesema fasihi ni kanzidata hivyo ni vyema tamaduni za nchi zikalindwa na kuendelezwa kwa maandishi  kwa  kuwaunga mkono wandishi chipukizi ili waweze kuwa na nguvu ya kuiendeleza kazi hiyo.

Amesema Zanzibar kwa miaka mingi imekuwa ikitoa waandishi mbalimbali mashuhuri wakwemo Bwana Mohamed Said Abdulla (BWANA MSA), Profesa  Said Ahmed, Bw Adam Shafi nk, ambaobwalikuwa ni Chem chem ya Fasihi ya Zanzibar na kupasua anga za Ulaya.

Mhe Riziki amesema Riwaya ya Fanani ni moja kati ya Riwaya bora katika zama hizi, kwani inawafunza na kuwakumbusha mambo mengi, pamoja na kuwatanabahisha masuala ya kale na ya sasa wa namna tofauti.

Amefahamisha kuwa  Riwaya ya Fanani imetoa na kuonesha na mafunzo kwa watoto wa kila rika, wa kike na wa kiume na kuwafafanulia juu ya raha na karaha za ulimwengu huu.

Mhe Riziki amesema kwa miaka ya hivi karibuni utamaduni wa kusoma vitabu umepungua kutokana na mvuvumko wa Tasnia ya TEHAMA, hivyo muda umefika wa kuufufua utamaduni huu kwa kuanzisha programu mbalimbali.

Aidha amewaomba wananchi kuisoma Riwaya hiyo kutokana na fasihi iliyotumika katika kuelimisha jamii ni miongoni mwa masuala mazima ya maisha ya mwanaandamu pamoja na  kuwakomboa wanawake.

"Mtoto hutizama kisogo cha mzazi wake"  siku zote watoto huweka miguu yao  pale palipoachwa alama ya nyayo za wazazi wao.

"Tusilaumu kizazi tulichonacho, ila tulaumu njia wanazopitia wazazi wao, ukiacha kitabu, kitasomwa kitabu, ukiacha simu utaperuziwa simu, ukiacha televisheni itatazamwa mpaka mtoto anyakuliwe na usingizi akiwa mbele ya kioo, kwa hivyo tuwe makini na teknolojia hii." Amesisitiza Mhe Riziki. 

Hivyo Mhe Riziki ametoa wito kwa waandishi na wanafasihi kwa ujumla kuzingatia dhima za fasihi ya mswahili kabla hawajazitoa kazi zao. 

Pia  Mhe.Riziki amempongeza Bi Zainab kwa ujasiri aliouonesha kwa kutunga Riwaya hiyo pamoja kueelezea kufurahishwa kwake kwa kuona Riwaya hiyo kuwa imetungwa na mwanamke.

Hata hivyo Mhe Waziri ametumia fursa hiyo kuiomba jamii kuungana na kushirikiana kwa  pamoja katika kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, kwani vitendo hivyo vimekuwa vikiathiri jamii ya walio wengi nchini.

Nae Kamishna wa Utamaduni Zanzibar Dr Omar Salum amesema dunia kila siku inabadilika, hivyo ni vyema yaliyoandikwa katika Riwaya hiyo kuyasoma kwa makini na kushirikiana ili yawe ni miongoni mwa  miongozo katika kuwalea vyema watoto wao.

Amesema Bi Zainab amekuwa akiendeleza utamaduni wa wazazi wao, hivyo amewaomba wananchi wengine wenye uwezo na vipaji kujitokeza kuandika na kutunga riwaya mbalombali ili kuendeleza urithi na utamaduni wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.