Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikabidhi nyenzo za kazi kwa Mkuu
wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo mara baada ya kukamilika kwa hafla ya uapisho
na ukaribisho kwa Wakuu wa Wilaya waliohamia katika Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongella akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo tarehe 30/01/2023. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkapa, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na Watendaji wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kukamilika
kwa hafla ya uapisho kwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongella na
kuwakarisha Wakuu wa Wilaya Bahi Mhe. Godwin Gondwe na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo. Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma amewaasa kusimamia viapo vyao.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Rosemary Senyamule amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald R. Mongella
pamoja na kuwapokea Wakuu wa Wilaya wapya wawili waliohamishiwa Mkoa wa Dodoma
kwenye hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa jengo la Mkapa zilipo Ofisi za Mkuu
wa Mkoa.
Mhe. Senyamule amewaasa
Wakuu hao wa Wilaya kuheshimu nafasi waliyopewa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu
Hassan kwani wameaminika kuitumikia nafasi hiyo. “Nafasi ya Ukuu wa Wilaya ina madaraka
na dhamana kubwa sana, ukiyatumia kwa tija yanaleta manufaa ila ukiyatumia
vibaya utakwenda kupata matokeo mabaya”
Aidha Mhe. Senyamule amesema
kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na nafasi waliyopewa wakuu hao ni kuja kuijenga Makao Makuu.
“Kuja Dodoma ni bahati kwakuwa
mnakuwa sehemu ya kujenga Makao Makuu ya nchi. Yeyote aliyekuja hapa, ajue
amepata nafasi ya kujenga Makao Makuu kwani viongozi wetu wakuu wana matarajio
makubwa na sisi. Mkoa umejipanga kuifanya Makao Makuu kama yalivyo matarajio ya
viongozi wetu” Mhe. Senyamule
Vilevile Mhe. Senyamule
amegusia changamoto zinazoukabili Mkoa wa Dodoma kwenye sekta ya elimu ikiwemo
utoro, ufaulu hafifu, ukosefu wa chakula shuleni na upungufu wa miundombinu ya
elimu na kuwaagiza Wakuu hao wapya kwenda kusimamia kikamilifu utatuzi wa changamoto
hizo kwa kushirikiana na watendaji na wenyeviti wa Vijiji na Kata.
“Halmashauri zetu zina
changamoto kubwa kwa upande wa elimu ambazo tunajitahidi kukabiliana nazo kwa
mwaka huu. Kwenye upungufu wa miundombinu, nimetoa maagizo kwa wenyeviti wa
Kata na Vijiji kukaa vikao na kukubaliana kujenga maboma mawili kwa kila Kijiji
kwa mwaka, nendeni mkasimamie agizo hili” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Naye Katibu Tawala wa Mkoa
wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga, amepata fursa ya kutoa neno kwa Wakuu hao wapya
wa Wilaya wakati wa hafla hiyo;
“Bahi imejipambanua vizuri
kwa elimu, miradi na mambo mengine mengi hivyo tunaamini Mkuu wa Wilaya Mpya
atakwenda kuendeleza hayo. Wilaya ya Mpwapwa bado ipo nyuma kwenye
uandikishwaji wa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza mwaka huu hivyo
tunategemea utakwenda kuhimiza zaidi. Tunategemea Wilaya iwe na vitendo Zaidi
kuliko nadharia” Dkt. Mganga
Katika salamu zao za
shukrani, wakuu wa Wilaya ya Chemba na Mpwapwa wameahidi kufanya kazi kwa
weledi na uaminifu kama viapo walivyoapa vinavyowataka huku wakitekeleza ilani
ya Chama Tawala pia wamesema kuwa dhamana waliyopewa ni deni kwa Mhe. Rais
aliyewaamini kwa kuwapa na fasi hizo na wanapaswa kulilipa. Wameahidi kuviishi
viapo vyao na kwenda kutekeleza maagizo yote ya Mkuu wa Mkoa huku wakiwa tayari
kutumika wakati wowote.
Uapisho huo umekwenda
sambamba na kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Munkunda
aliyehamishiwa katika Wilaya ya Temeke
Mkoani Dar es Salaam. Wengine waliokaribishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe.
Godwin Gondwe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo.
No comments:
Post a Comment