Habari za Punde

Uzinduzi wa Vikundi Vya Ujasiriamali

Na Maulid Yussuf WMJJWW Zanzibar 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amewataka wanawake kushirikiana kwa pamoja na kusaidiana ili kujiletea maendeleo.

Mhe Riziki ameyasema hayo wakati akizindua vikundi vitatu vya ujasiriamali vilivyokuwa chini ya Kampuni ya Amina Brown Collection, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Palm Tree Mombasa Mjini Unguja amesema maendeleo ya kweli yanaletwa na wanawake hivyo wanaposhirikiana wataweza kujiinua katika kujikwamua na maisha.

Mhe Riziki amempongeza ndugu Amina Naufal (Zanzibar makeup Artist) ambae ndie mmiliki wa Kampuni hiyo kwa ubunifu alioufanya wa kuwakutanisha wanawake wenziwe na kuwashajiisha katika kujiajiri.

"Mwenye nacho amsaidie asiekuwa na nacho, na kitu kizuri gawana na mwenzako, hii iteleta upendo na mfanikio kwa wengine, na sio kukaa kumsema na kumcheka." Amesisitiza Mhe. Riziki.

Kuhusu suala la upatikanaji wa mikopo Mhe.Riziki amewataka kufika katika wizara husika na kufuata masharti huku akiwaahidi kuwa  Wizara ya Maendeleo ya Jamii itajitahidi kuwafuatilia ili kuona wanawake wanawake  wanapata mikopo.

Pia amewataka kujitahidi Kutengeneza bidhaa zenye ubora ili kuwa rahisi katika kuwapatia masoko.

Hata hivyo Mhe.Riziki amewataka wanawake wote nchini kuungana katika kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwani vimekuwa vikiwaathiri zaidi watoto.

Akisoma Risala ya Mkurugenzi na Muanzilishi wa Kampuni ya Amina Brown Colour Collection, Mjumbe wa kampuni hiyo ndugu Ahlam Abdalla Azzan amesema ndugu Amina ni mzalendo na amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anatafuta fursa za kutosha na kushirikiana na wanawake na vijana katika kuleta ubunifu wa kimaendeleo ndani na nje ya Zanzibar. 

Amesema tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo wameweza kuzalisha ajira zaidi ya wanawake 150 kwa kuwapa ujuzi wa masuala ya upambaji mabiharusi, wasanii wakubwa pamoja na kukuza vipaji mbalimbali vya sanaa na kuwatafutia masoko.

Amesema lengo lao ni kuendelea kuzalisha fursa kwa wanawake na vijana kuweza kujikwamua kiuchumi, kujikomboa na changamoto ya wa  ajira pamoja na kunyanyua vipaji mbalimbali. 

Hata hivyo ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha wanawake na vijana wanajikomboa na ugumu wa maisha kupitia vipaji walivyokuwa navyo.

Hata hivyo ameiomba Serikali kutoa vipaombele kwa vikundi vya wanawake na wajasiriamali wadogo wadogo na vijana katija kuwapatia mikopo nafuu pamoja na kuwatafutia masoko ili waweze kufikia malengo na kuchangia pato la nchi.

Kmpuni ya Amina Brown Colour Collection, imeanzishwa mwaka 2015 na  kusajiliwa rasmi  Novemba 2019, ambapo uzinduzi wa vikundi vitatu umenda sambamba na burudani ya muziki wa taarab.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.