RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka vijana kuzitumia fursa zilizopo na zitakazoletwa na Serikali na
Wadau mbalimbali wa Maendeleo kwa ajili ya Maendeleo na Ustawi wao na Taifa kwa
ujumla.
Alisema vijana ni nguvu kazi kwa taifa lolote duniani, ambayo inahitaji
kuandaliwa vema kwa faida za baadae.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo huko Maisara
Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza na vijana wa makundi
tofauti kwenye uzinduzi wa mradi wa “Kijana Nahodha” unaofadhiliwa na Shirika
la USAID la Marekani.
Alisema mradi huo unaunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye utekelezaji wa mipango ya maendeleo
ya kitaifa ikiwemo dira ya 2050, mpango wa taifa wa maendeleo 2026 na Ilani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 -2025.
Alisema kundi kubwa la vijana duniani kote limekuwa likikabiliwa na changamoto
nyingi ikiwemo ukosefu wa ajira, matumizi ya dawa za kulevya, mimba na ndoa za
umri mdogo, UKIMWI, Afya ya Akili, ukatili na udhalilishaji wa kijinsia pamoja
na matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Dk. Mwinyi alizitaka Wizara zote zinazoguswa
na mradi huo kushiriki na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake ili kufikia
malengo yaliyokusudiwa kwa kuwaandaa na kuwasimamia vijana kuhakikisha shughuli
watakazozianzisha zinakua endelevu hata baada ya kukamilika Mradi.
Akizungumzia mabaraza ya vijana Dk. Mwinyi
alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inasimamia uendeshaji wa Baraza la Vijana la Zanzibar
kuanzia ngazi ya Shehia hadi taifa pia alisema baraza hili ni chombo
kinachowaunganisha vijana nchini ili kupaza sauti zao kwenye masuala mbalimbali
yanayohusu maslahi yao pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii.
Alieleza mabaraza hayo yamechangia kuanzishwa
vituo vya mafunzo ya vijana maeneo ya Bweleo na Pangeni kwa Unguja na Weni na
Mjini Ole kwa Pemba kwa kuwaandaa vijana kupata maarifa na umahiri wa kukabiliana na changamoto kwenye
makuzi yao.
Akizungumzia fedha za ahueni ya
Uviko isiyo na riba, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ilitoa fedha hiyo
kwaajili ya mikopo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, kujenga vituo maalumu vya
wajasiriamali kwa kila Wilaya pamoja na kuwapatia wananchi vifaa vya uvuvi
zikiwemo boti na vifaa vyengine vya uvuvi wa kisasa, vifaa kwa wakulima wa
mwani kwa vijana na kinamama. Alisema Serikali imeongeza uwekezaji wa miradi
mbalimbali ikiwemo ya binafsi, uimarishaji wa shughuli za uchumi wa buluu
ikiwemo kuendeleza sekta ya utalii, kukuza uchumi wa nchi na kuongeza fursa za
ajira ambazo vijana ni miongoni mwa walengwa wakuu.
Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita aliwaomba wadau wa
maendeleo kuendelea kuiungamkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwekeza
zaidi kwenye miradi inayowahusisha vijana ili kuwakomboa na changamoto
zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ajira wapate kujitegemea.
Naye, Mkuu
wa Mradi wa Kijana Nahodha, Dk. Tuhuma Tuli alieleza mradi ni sekta mtambuka amabao utahusisha ajira kwenye sekta za elimu,
kilimo, utawala bora na afya kwa unalengo la kuwajengea uwezo vijana wenye umri
kati ya miaka 15-25.
Alisema mradi pia imelenga kuwajengea uwezo vijana,
kuwasaidia upatikanaji ubora wa stadi mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ufundi, kuboresha
uelewa wa afya ya akili kupitia zana za elimu ya kidijitali zinazoongozwa na
watu binafsi na kuimarisha njia za wazi za mawasiliano kati ya vijana na
serikali ili kuinua sauti za vijana katika maisha ya kiraia, siasa, na utungaji
sera.
Kwa upande wake Mkururgenzi Mkazi wa USAID, Kate
Somvongsiri alisema, kupitia mradi wa Kijana Nahodha, vijana watakuwa na uwezo
wa kujifunza masuala mbalimbali, kuongeza maarifa na stadi za kuendesha
biashara, misaada kutoka kwa familia zao, jamii, na serikali ili wapate fursa
kupitia elimu.
Mradi wa Kijana Nahodha wenye kaulimbiu “Kijana Nahodha mpango mzima”. Unatarajia kuwafikia vijana 45,000 kwa
Tanzania nzima ambapo kwa Zanzibar unatarajiwa kuwafikia vijana 15,000 Unguja
na Pemba.
IDARA YA
MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment