Habari za Punde

Serikali Yaanza Maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Christian Omolo, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hafla ya uzinduzi wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango, Aprili 3, 2023, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakuu wa Idara na Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango, wakifuatilia kwa karibu mkutano na waandishi wa habari kuhusu hafla ya uzinduzi wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Aprili 3, 2023, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

Na Farida Ramadhani, Dodoma

Wizara ya Fedha na Mipango imesema kuwa Serikali imeanza mchakato wa kuandaa Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo (Vision 2050), ambayo itatoa maono na kuweka malengo ya Taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

 

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Christian Omolo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hafla ya uzinduzi wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Aprili 3, 2023 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

 

Bi. Omolo alisema Maandalizi ya Dira mpya ya 2050 yanakidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuisha kwa kipindi cha utekelezaji wa Dira iliyopo sasa ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, inayotarajiwa kumaliza muda wake baada ya miaka miwili ijayo.

 

“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 utekelezaji wake utafikia tamati mwaka 2025 ambapo hadi sasa utekelezaji wake umeliwezeshaTaifa kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali hususan za kijamii, kiuchumi na kisiasa”, alisema Bi. Omolo.

 

Alisema kuwa historia ya upangaji wa mipango nchini imeanza kuanzia nchi ilivyopata uhuru ambapo matamanio yalikuwa kupambana na maadui watatu wa Taifa, ukiwemo ujinga, umaskini na maradhi.

 

“Mwaka 1964, Tanzania ilifanikiwa kuandaa Mpango wa kwanza wa Muda Mrefu wa miaka 15 ambao ndani ya utekelezaji wake uliimarishwa na Azimio la Arusha la mwaka 1967 na Mpango wa Pili wa Muda mrefu uliandaliwa Mwaka 1981  ”, alibainisha Bi. Omolo.

 

Alisema utekelezaji wa mipango hii ulienda sambamba na utekelezaji wa programu mbalimbali zilizosimamiwa na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa, (IMF) zikiwa na lengo la kuleta utulivu wa kiuchumi na marekebisho ya kimuundo nchini.

 

“Katika kufanikisha malengo yaliyopangwa, Serikali ilianza mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa (TDV 2025) mwaka 1995 ambao ulikamilika mwaka 2000”, alieleza Bi. Omolo.

 

Alisema utekelezaji wa Dira hiyo ulianza kupitia programu za kupunguza umaskini kama Mkakati wa Kupunguza Umaskini (PRS I) mwaka 1999/2000 - 2002/03, unaojulikana kama Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA I) mwaka 2004/05 - 2009/10 na MKUKUTA II mwaka 2010/11 -i 2014/15.

 

Bi. Omolo alibainisha kuwa mwaka 2009/10, Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kupitia mikakati na programu za maendeleo na kubaini kuwa kuna uhitaji wa Taifa kuanza kupanga vibaumbele vya nchi ambapo Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu  (LTPP) 2011/12 - 2025/26) uliundwa.

 

Aidha, Alitoa rai kwa wadau wote kushiriki kwa kiasi kikubwa kutoa mchango wao utakaowezesha kuandaliwa kwa Dira mpya yenye maono ya watanzania kwa miaka 25 ijayo kwa kuwa kufanikisha kwa zoezi la maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wadau wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.