KATIKA kuhakikisha lengo la ushiriki sawa wa wanawake kwenye nafasi za uongozi linafikiwa, wanawake wenye nia ya kugombea na kushika nafasi hizo wametakiwa kutumia muda wao kukaa karibu na jamii zao ili kubaini changamoto zinazowakabili wananchi na kusaidia kuzitaftia ufumbuzi badala ya kusubiri kipindi cha uchaguzi.
Imeelezwa kuwa suala la ushiriki kugombea nafasi za uongozi ni mchakato endelevu ambao unahitaji maadalizi ya muda mrefu bila kusubiri kufanya maandalizi hayo kipindi cha uchaguzi kinapokaribia jambo ambalo linapelekea jamii kukosa inami nao.
Hayo yameelezwa na wadau wa usawa wa kijinsia wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wanawake 35 wenye dhamira ya kugombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa kisiwani Pemba yaliyoandaliwa na Chama Cha Wandhishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway kutambua misingi, taratibu, wajibu na hatua muhimu za kufuatwa kabla na wakati wa kugombea ili kuwa kiongozi bora katika jamii.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Salum Suleiman Ali, kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) alisema wanawake wanayo nguvu ya ushawishi na iwapo watajua namna ya kuitumia kwa kujenga hoja na kuwa karibu na jamii itawasaidia kufikia malengo na kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali bila vikwazo.
“Wanawake lazima kwanza tuwe na uwezo wa kujitayarisha kiuongozi ikiwemo kuyaacha baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutumika kukubomoa. Kisha utambue changamoto zilizopo katika jamii na kubaini fursa zilizopo za kuweza kutatua changamoto hizo,” alieleza Dkt. Salum.
Aidha alisema ili kufikia lengo hilo kila mwanamke anatakiwa kuwa jeshi la kumlinda na kumuongoza mwenzake kwenye masuala ya uongozi ili kujenga heshima ya wanawake wote kwenye uongozi bila kuharibu heshima ya wanawake wengine.
“Uongozi kwenye jimbo huendi kumtawala mtu. Kubwa ni kwenda kusikiliza matatizo na changamoto za watu na kuisaidia jamii kuondokana na matatizo hayo kazi ambayo inaweza kufanywa muda wowote na kila mmoja awe ni mwanamke au mwanaume hivyo ili uweze kufanikisha hilo lazima kwanza uwe karibu na watu wako mapema ili kuzijua vizuri shida zao kwa undani,” alieleza Dkt. Salum Suleiman Ali.
Aidha alifahamisha, “mafunzo haya yamekuja mapema ambapo bado miaka miwili kuelekea uchaguzi mkuu kwasababu kuna mambo muhimu unatakiwa kuyaanza mapema na sio kusubiri uchaguzi umefika ndipo uanze mchakato kwasababu kwenye siasa sio ujanja bali ni mikakati bora inayolenga kutetea wananchi unaowaongoza.”
Mapema mratibu wa TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanawake kushikamana bila kujali tofauti za vyama vya siasa lengo likiwa ni kufanikisha kupata idadi kubwa ya wanawake wanaoingia katika nafasi za uongozi.
Alieleza, “kila mmoja wetu humu tunataka angalau awafikie wanawake wengine 20 kwenye vyama vyetu na jamii zetu kutoa elimu ili tupate uwakilishi wa wanawake wengi walio bora na wenye uthubutu wa kusimama na kuongoza katika nafasi mbalimbali kwa kufuata misingi na maadili yanayotakiwa kwa kiongozi bora.”
Kwa upande wake mkurugenzi wa Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) akizungumzia kuhusu mafunzo hayo yaliyoandaliwa kupitia mradi wa Wanawake na uongozi alisema yanalenga kuwaandaa wanawake weye nia ya kugombea nafasi hizo kuwa na uwezo wa kusimama kutatua changamoto zinazoikabili jamii kabla ya kugombea katika chaguzi mbalimbali.
“Mafunzo haya yameletwa mapema ili tuanze kutumia ujuzi huu tuliofundishwa kufanya kwa vitendo kwenye jamii kwa kukaa karibu nao kuzijua changamoto zao ili waamini na kuwaunga mkono katika jambo mnalofanya kuliko kukaa na kusubiri kipindi cha uchaguzi ndipo unaenda kwenye jamii kutaka wakuchague kuwa kiongozi wao,” alieleza mkurugenzi huyo.
Zainab Mussa Bakar mmoja wa washiriki kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Pemba aliwataka wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuwekeza nguvu katika kujijengea uwezo binafsi ikiwemo kujiendeleza kielimu ili kuepukana na changamoto za udhalilishaji wanazokumbana nazo kipindi cha uchaguzi.
Alisema, “wanamke tunatakiwa tujiamini na tujitahidi tuwe na uwezo binafsi hasa kujiendeleza kielimu, tusitegemee mtu katika nafasi za uongozi na badala yake tutegemee zaidi nguvu na uwezo wetu kwani kumtegemea mtu atakapoona unafanikiwa kumzidi atatafufa njia ya kukushusha.”
Mafunzo haya maalum ya kuwajengea uwezo wanawake wenye dhamira ya kugombea nafasi za uongozi yanakuja baada ya kufanyika kwa mikutano ya uhamasishaji kwenye Shehia iliyofanywa na Wahamasihaji Jamii kuhusu umuhimu wa wanawake kudai na kushiriki kwenye nafasi za uongozi na wanawake hao kuhamasika kuwa tayari kugombea nafasi hizo.
No comments:
Post a Comment