Na. Maulid Yussuf -Zanzibar.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amewataka waislamu nchini kuisoma Qur-aan na kuifahamu maudhui yake ili kujiepusha na matendo maovu.
Mhe Riziki ameyasema hayo wakati wa mashindano ya 10 ya Kuhifadhi Qur-aan ya akina mama wa Kitope, yaliyofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kitabu cha Qur-aan kimefundisha masuala mbalimbali ya mwenendo mzima wa maisha hivyo watakapokijua maudhui yake na kuyafuata kwa usahihi wataweza kuondokana na vitendo viovu ikiwemo udhalilishaji.
Aidha amewashuri walimu wa madrasa kufundisha Qur-aan kwa njia za kisasa za mutandao ya simu, projector au computer ili wanaposoma wanafunzi wawaone masheikh wakubwa namna wanavyosoma Qur-aan ili waweze kuiga kutoka kwao, badala ya kutumia mitandao hiyo kwa mambo yasiofaa.
Hata hivyo Mhe Riziki Amewapongeza kina mama waliohifadhi Qur-aan kuanzia juzuu ya pili hadi juzuu ya ishirini na kuwataka kina mama wengine kufika katika madrasa mbalimbali ili kujifunza kwa lengo la kukitukuza kitabu cha Allah na kupata fadhila kutoka kwa mola wao.
Naye kiongozi wa kamati ya mashindano ya kuhifadhi Qur-aan Ukhty Khadija Suleiman Mohd amemshkuru Mhe Riziki kwa kuweza kutenga muda wake kukubali kuhudhuria katika mashindano hayo ambayo yanawapa hamasa wanawake wengine kujiunga na madrasa mbalimbali.
Akisoma risala ya mashindano hayo Ukhty Shufaa Khamis amesema tokea kuanzishwa madrasa yao mwaka 2002 wamekuwa wakifanya mashindano ya kuhifadhisha Qur-aan kwa watu wazima na vijana ambapo ni mafanikio makubwa yamepatikana kwani kitokana na Kina mama wengi kujiunga na madrasa yao.
Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto balimbali ikiwemo uhaba wa vyoo pamona na ukosefu wa umeme huku wakimuomba mhe Riziki kufika kuwatembelea ndani ya Madrasa yao.
Mshindi wa mashindano hayo kwa juzuu 20 bi Asha Masoud amewaomba kina mama wenziwe kuacha kukaa katika baraza zisizo na maana na badala yake wajiunge na madrasa ili kusoma Qur-aan na kuweza kupata fadhila za Allah.
Mashindano hayo ya kuhifadhi Qur-aan yameshirikisha juzuu 2, 4, 6, 8, 10, 13, 18 na juzuu 20 ambapo washindi wa kwanza kwa kila juzuu wamepatiwa zawadi pamoja na pesa taslim.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO.
No comments:
Post a Comment