Habari za Punde

Waziri Mhe. Jafo Aridhishwa nac Mradi Wilayani Mkalama Ahimiza Kasi ya Utekelezaji

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mpambala Lugongo Halmashauri ya Mkalama mkoani Singida Mei 06, 2023 alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) unaotekelezwa katika halmashauri hiyo na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikagua ukarabati wa josho la kuogeshea mifugo Mei 06, 2023 katika Kijiji cha Nyahaa Halmashauri ya Mkalama mkoani Singida ambalo linakarabatiwa kupitia Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) unaotekelezwa katika halmashauri hiyo na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifurahia asali iliyorinwa na wanakikundi katika msitu wa Chemchem katika kijiji cha Mpambala Mei 06, 2023 kupitia mradi wa ufugaji nyuki ili kuhifadhi mazingira unaotekelezwa kupitia Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) unaotekelezwa katika halmashauri hiyo na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kimazingira inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mkalama mkoani Singida ikiwemo ukarabati wa josho, ufugaji wa nyuki na jengo la kuchakata nafaka.

Hayo yamejiri Mei 06, 2023 wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) unaotekelezwa katika halmashauri hiyo na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo alisema kuwa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi katika maeneo yenye changamoto za kimazingira ili wananchi waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato huku wakihifadhi mazingira.

Akikagua ukarabati wa josho linalohusisha ukarabati wa kibanio cha josho, chanjo na tenki la maji ambalo lilikuwa limechanika, Dkt. Jafo aliwahimiza wataalamu wilayani humo kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

“Kwa hali ninayoiona hapa mradi utakuwa mzuri na utawahudumia wananchi lakini unapokamilika kuna stage (hatua) ya pili yaani matumizi ya mradi wenyewe kuna hii sehemu ya kuogeshea na sehemu ya maji kama kikundi muweke utaratibu mzuri wa usimamizi ili kuhakikisha mifugo yote inaogeshwa hapa ili mradi uweze kujiendesha maana sidhani kama kila mara Halmashauri ilete fedha hapa,“ alisisitiza.

Katika hatua nyingine akiwa ziarani wilayani humo Dkt. Jafo aliwatembelea wanakikundi cha ufugaji wa nyuki katika msitu wa Chemchem uliopo kijiji cha Mpambala ambacho kimepatiwa mizinga zaidi ya 300.

Mradi huo unahusisha pia vifaa vya kuchakatia na kupakia asali pamoja na mavazi ya kurinia ambavyo vimetolewa na Serikali ambapo pamoja na kuwapatia asali lakini pia wanahifadhi msitu.

Akizungumza na wanakikundi hao Waziri Jafo aliwaongeza kwa kuhifadhi mazingira na kuwachagiza kuhusu baishara ya kaboni ambayo tayari kanuni na mwongozo wake umeshatangazwa.

Aidha, Waziri alikagua hatua za ujenzi wa jengo la kuchakata nafaka katika kijiji cha Lugongo ambalo litajumuisha pia usimamikaji wa kinu cha kuchakata nafaka ambao ukikamilika utawawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali aliishukuru Serikali kwa kuratibu miradi hiyo akisema itasaidia wananchi kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi wilayani humo.

Alimshukuru Waziri Jafo kwa kufanya ziara ya kutembela na kukagua mradi huo katika wilaya hiyo na kusema imeleta tija.

Baadhi ya wananchi akiwemo Bw. Fanuel Kali Mradi wa LDFS umewanufaisha kwani kupitia elimu waliyoipita kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira pia wanaitoa kwa wananchi wenzao.

Waliiomba msitu huo utambulike na kuingizwa katika biashara ya kaboni ili waweze kunufaika pamoja na kuendelea kuutunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mradi wa LDFS unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) unatekelezwa pia katika Halmashauri zingine ikiwemi Nzega (Tabora), Magu (Mwanza), Kondoa (Dodoma) na Micheweni (Kaskazini, Pemba).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.