Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameonesha kuridhishwa na uzingatiaji wa Kanuni na Sheria ya Mazingira katika Bandari ya Mtwara.
Hayo yamejiri wakati wa ziara
ya kikazi ya Dkt. Jafo ya kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira eneo la
utunzaji na usafirishaji wa makaa ya mawe zinazofanyika katika bandari hiyo.
Ameupongeza uongozi wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mkoani humo kwa kushirikiana na Kampuni
ya Ruvuma Coal kwa hatua ya kulinda mazingira.
Aidha, Waziri Jafo amesema
ameridhishwa na namna ambavyo wameweka uzio kuzunguka eneo yanapohifadhiwa
makaa ya mawe ili kudhibiti vumbi lisisambae na kuathiri wananchi.
“Binafsi nikiwa na dhamana ya
kusimamia sekta ya mazingira nimeridhika kwani mmetekeleza maelekezo yangu
niliyoyatoa nilipofanya ziara katika siku zilizopita,” amesema Dkt. Jafo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu biashara.
Pia, amemshukuru kwa kuruhusu Bandari
ya Mtwara kutumika kusafirishia bidhaa ya makaa hayo yam awe akisema kuwa inaliingizia
taifa kipato na kukuza uchumi.
Kuhusu maelekezo
yaliyotolewa na Waziri Jafo, Ahmed ameahidi kwa
kushirikiana na wataalamu kutoka ofisi yake kuwasimamia wawekezaji ili kuwa na
biashara isiyo na madhara kwa wananchi.
Nae Meneja Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini Mhandisi Boniphace Guni ameahidi kusimamia agizo hilo ili liweze kutekelezeka kwa muda uliopangwa wakati Meneja wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Jitegemee Bw. Boscow Mabena ameahidi kuwa watafuata ushauri wa wataalamu ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Itakumbukwa Desemba 20, 2021 Waziri Jafo alipofanya ziara bandarini hapo alitoa muda wa miezi sita kwa uongozi kufanya marekebisho ya dosari za kimazingira zilizobainika ikiwemo kuandaa eneo maalumu lililokidhi vigezo litakalotumika kuhifadhi makaa ya mawe yanayosafirishwa.
No comments:
Post a Comment