SERIKALI ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imesema itaendelea kufanya utafiti utakaoonesha njia bora zaidi za
uvunaji wa maji ya mvua pamoja na maji kwenye mabwawa, ili kutafuta vyanzo
vyengine vya maji na hatimae kuongeza ufanisi kwenye sekta ya maji nchini kwa
manufaa ya wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo alipofungua Kongamano la Maji
kwenye ukumbi wa hoteli ya Verde, Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dk. Mwinyi, aliiasa jamii kuendelea kuilinda
miundombinu ya maji na kuvilinda vyanzo vya maji vilivyopo kwa kuviepusha na
shughuli zao zikiwemo ujenzi na kuanzisha makazi.
Aidha, aliitaka jamii kuendelea kuimarisha
mazingira kwa kupanda miti ambayo ni muhimu kwa upatikanaji wa mvua.
Pia, Dk. Mwinyi aliwaagiza viongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na
Madini, kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na watafiti wanaofanya utafiti
kwenye sekta hiyo, ili wawe na mipango madhubuti ya kukusanya na kutumia
matokeo ya utafiti unaofanywa Zanzibar kwa maendeleo ya taifa.
Halikadhalika
aliutaka uongozi wa Wizara hiyo, kuandaa mpango
wa muda mrefu wa Sekta ya Maji ili usaidie kubainisha miongozo ya sekta hiyo na
hatimae kupunguza changamoto zilizopo.
Vilevile, Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Wizara hiyo
kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, kuandaa utaratibu wa
kuyatambua na kuyapatia hatimiliki maeneo yote ya vyanzo vya maji, Zanzibar.
Alisema, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya maji kwa
kutekeleza miradi mikubwa kama ilivyopangwa na kuelekezwa kwenye Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, kufuatia
ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Pia, alieleza miradi mikubwa ya maji inayoendelezwa za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia fedha za Mkopo wa Ahueni ya UVIKO
kutoka shirika la Fedha duniani (IMF) itatoa mchango mkubwa na kuondoa
changamoto za maji zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania, Juma Aweso, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Maryprisca
Mahundi alieleza Serikali ya SMT kupitia Wizara aiko hatua za mwisho za
maangali ya miradi yake mikupwa ya mumtua ndoo ya maji mama kichwani
Naye, Waziri wa Maji Nishati na Madini, Shaibu Hassan
Kaduara, aleleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada zake
za kuwafikishia wananchi huduma za maji safi na salama nakueleza mwezi Septemba
mwaka huu Serikali kwa mara ya kwanza inatarajia kuzindua nangi la maji la lita
milioni 32, ambayo litasambaza maji kwenye maeneo mengi ya Zanzibar.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment