Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Azungumza na Balozi wa Marekani

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akiwa na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Bw. Michael Anthony Battle, na viongozi mbalimbali katika ghafla ya chakula cha mchana na mazungumzo yalioandaliwa na ofisi ya Ubalozi wa Marekani iliyofanyika katika kituo cha usimamizi na kujifundishia lugha ya Kiingereza kilichopo Chachani Chake chake  Kisiwani Pemba leo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman ameishukuru Serikali ya Marekani kwa kuendeleza azma ya kuungamkono maendeleo ya Visiwa vya Unguja na Pemba, na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Othman ametoa shukran hizo leo huko Kituo cha Wamarekani 'American Corner' kiliopo Chachani Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani Nchini, Bw. Michael Anthony Battle.

Amesema azma hiyo imedhihiri pale Balozi Battle alipofika na Ujumbe wake kisiwani Pemba, kufuatia Ahadi yake aliyoitoa Mapema Mwaka huu, wakati alipomtembelea Mheshimiwa Othman Ofisini kwake, Migombani Mjini Unguja.

Mheshimiwa Othman amesema kuwa Serikali ya Zanzibar imepata matumaini na haina budi kushukuru kwa dhati, baada ya Ahadi hiyo ya Balozi Battle na Serikali ya Marekani kwa ujumla, ya kufika na kujionea Mazingira ya Kisiwa cha Pemba ili kuungamkono hatua mbali mbali za maendeleo ya watu, jamii na Serikali kwa ujumla.

Aidha anesema Marekani na Zanzibar ni Nchi Mbili zenye uhusiano mkubwa, wa tangu, na wa muda mrefu, hivyo ni faraja kuona zinaendelea kushikana- mikono katika harakati kupitia nyanj mbali mbali zikiwemo za maendeleo ya kiuchumi, utawala wa sheria na uwekezaji.

Mheshimiwa Othman, katika Maongezi hayo yaliyoambatana na Chakula cha Mchana, kilichoandaliwa na Ubalozi wa Marekani, na kuwajumuisha Viongozi na Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Zanzibar, amemkaribisha Balozi wa Marekani Pemba na kumtaka ajisikie yupo nyumbani na kujionea utajiri wa asili ukiwemo wa Mandhari ya kuvutia Kisiwani hapa.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani Nchini, Bw. Michael Anthony Battle ameeleza kwamba wameamua kutekeleza miadi hiyo waliyoiwekahapo kabla akiamini kwamba Nchi yake inao wajibu wa kuhamasisha maendeleo ya Afrika, Tanzania, na Zanzibar yote, bila kuiweka kando Pemba.

Katika ahadi yake, Bw. Battle amesema Marekani itaweza kusaidia na kutoa fursa mbali mbali za kuiendeleza Zanzibar, ikiwemo Mafunzo kwa Askari 12 Wanamaji na Wanaanga kutoka Visiwani hapa.

Amesema Marekani imeridhishwa na hatua ya Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar, na inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Serikali iliyopo, ya Umoja wa Kitaifa (GNU).

Katika Ujumbe wake, Balozi Battle ameambatana na Maafisa mbali mbali, akiwemo Afisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Marekani Tanzania, Bw. Mussa Ali Shehe.


Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Septemba 19, 2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.