Habari za Punde

Wazazi wa kiume wahimizwa kufuatilia elimu ya afya ya uzazi

 NA FAUZIA MUSSA  Maelezo

KINABABA wameshauriwa kufuatana na wenza wao wakati wanapokwenda kliniki kupata huduma za mama na mtoto ili kujua afya zao.  

Muuguzi Mkunga Hospital ya Mpendae Habiba Shaaban Nassor alieleza hayo wakati akitoa elimu ya Afya ya uzazi kwa wababa wa Shehia ya Mpendae na Vijiji jirani huko hospital ya Mpendae Wilaya ya Magharibi 'B'.

Alisema kufanya hivyo kunawapatia fursa ya kupata elimu hiyo wakati wenza wao wanapokuwa wajawazito.

Aidha alisema baadhi ya wababa hawana elimu ya kutosha juu ya elimu ya Afya ya uzazi na kupelekea kutotekeleza maagizo yanayotolewa na Serikali jambo linalorejesha  nyuma juhudi za serikali katika kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto.

Akizungumzia kuhusu kina mama wanaobeba ujauzito kabla ya ndoa aliwataka kutokuvunjika moyo kwani wanaweza kufika vituoni na kupatiwa huduma bila ya kuwa na wenzawao.

"Nnasisitiza kinababa muwasindikize wenzawenu lakini simaanishi  waliobeba ujauzito nje ya ndoa kuwa hawatohudumiwa kwa kukosa kuja na wenzawao Bali wanachotakiwa nikujieleza tu watakapofika vituoni"

Alibainisha kuwa mara tu wajawazito na wenzawao wanapofika vituo vya afya wauguzi na wakunga hutekeleza jukumu  la kuwapatia elimu ya kuwajengea uelewa juu ya mambo mbalimbali ya Afya ya uzazi ili kuepusha madhara kwa mama na mtoto.

Hata hivyo alibainisha kuwa kupitia elimu hiyo  mama wajawazito na wenzawao hupata fursa ya  kutambua dalili hatarishi kwa mama mjamzito pamoja na kujua wakati stahiki wa  kufika katika vituo vya Afya (kliniki).

Aidha aliwasisitiza kinababa kufanya haraka ya kuwapeleka hospitali mara tu dalili hatarishi zinapojitokeza ikiwemo tumbo kuuma chini ya kitovu, kutokwa na damu ukeni, kichwa kuuma, kizunguzungu, pamoja na kiza cha macho.

"Tuwe makini sana hata kama utaona damu  ndogondogo jitahidi uwahi kituo cha Afya "alisistiza.

Sambamba na hayo muuguzi huyo  aliwasisitiza kinababa kuwalazimisha wenza wao kula vyakula vinavyojenga mwili ikiwemo vyakula vya pwani ,mboga matunda pamoja na kuwakemea kula vitu kama udongo kwani huhatarisha afya ya mama na mtoto aliyekuwepo tumboni.

Aidha aliwashauri kinababa kuwa wavumilivu katika kipindi hicho cha mpito pamoja na  kuwasaidia wenza wao kazi za ndani kwani kufanya kazi nzito na ngumu kunachangia  kuharibika Kwa ujauzito.

Awali muuguzi huyo alimshukuru Rais wa Zanibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kupitia Wizara ya Afya kwa kuboresha huduma za mama na mtoto Unguja na Pemba na kuitaka jamii kutumia fursa hiyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza vifo visivyotarajiwa vya mama na mtoto.

Nao baadhi ya kinababa waliofatana na wenza wao walisema ni jambo la msingi kwa kinababa wengine kuiga mfano huo ambao unapelekea kuonesha mapenzi kwa mwenza na kujua matatizo anayopitia wakati wa ujauzito wake.

 Ali Salum Tamim, Issa Hassan Abdalla na Suleiman Abass Mustafa waliahidi kuwa  mabalozi wazuri kuwahamasisha kina baba wenzao na kuahidi kuifanyia kazi elimu hiyo ili kuleta  mabadiliko ya uzazi kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla hasa katika kupunguza takwimu za vifo vya mama na watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.