Habari za Punde

Mhe Hemed ahudhuria Maulidi Tanga


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na Waumini wa Dini ya kiislamu katika Hafla ya kusherehekea Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) iliyoandaliwa na Almadrasatu Saqafatul Islamiyya Takniya iliyofanyika Tanga Barabara ya Tisa.

 

Katika Hafla hiyo iliyopambwa kwa Kasidah na Milango ya Maulid ilitanguliwa na Dua ya kuwarehemu wazee waliotangulia mbele ya haki.

 

Akitoa Salamu zake katika hafla hiyo Mhe. Hemed amewataka wazazi na walezi kuwasimamia watoto kupata elimu itakayowasaidia kumjua Mola wao na kujua mafundisho ya Dini yao aliyokuja nayo Mtume Muhammad (S.A.W)

 

Amesema elimu bora na yenye manufaa hupatikana kwa kutanguliza nidhamu na adabu njema hatua ambayo itasaidia kuzalisha Viongozi bora watakaolisimamia Taifa wakiwa na hofu ya Mungu.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza suala la umoja na mshikamano katika jamii na kueleza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anasaidia jamii hasa makundi maalum ikiwemo Mayatima, wajane, wazee na wenye ulemavu hatua ambayo itasaidia kuongeza mapenzi katika Jamii.

 

 

……………………………..

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

10/10/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.