Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali itaendelea kutekeleza kwa ufanisi mikakati muhimu inayohakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, kwa wananchi wa mijini na vijijini, ili kufanikisha Mipango ya Maendeleo na Kukuza Uchumi wa Nchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akiwahutubia viongozi na wananchi wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, huko Chamanangwe, Shehia ya Kiuyu-Minungwini, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema, Serikali inaendelea na Utekelezaji wa Mikakati hiyo ambayo imejiwekea, kupitia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050, kwa dhamira pia ya kutambua kuwa, maji ni sehemu ya uhai, afya na haki ya msingi ya binadamu.
Akibainisha Mikakati ambayo ni pamoja na raslimali hiyo muhimu amesema, hadi kufikia Mwezi wa Machi 2023, hali ya uzalishaji wa maji Nchini imeendelea kuimarika, kwa kufikia asilimia 67 visiwa vya Unguja na Pemba, ikilinganishwa na asilimia 56 iliyofikiwa mwezi Machi 2022, huku Kiwango cha Uzalishaji-maji kikitarajiwa kuongezeka na kufikia wastani wa asilimia 75 ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2023.
“Ni dhahiri kwamba mahitaji ya maji Nchini yameendelea kukua, hivyo ni budi kila mmoja wetu kuyatunza na kuyatumia kwa uangalifu, sambamba na kuvitunza vyanzo vyenyewe; kutokana na ukweli huo, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeo, pamoja na Asasi za Kiraia, tunao wajibu mkubwa wa kuwawezesha wakulima, ili kuendeleza juhudi za uzalishaji wa chakula, na hatimaye kuongeza tija kwa maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla, kwaajili pia ya kuiwezesha Nchi kujitosheleza kwa chakula, huku tukizingatia matumizi bora na endelevu ya maji”.
Mheshimiwa Othman akifafanua zaidi Mikakakati ya Maendeleo ya Kilimo-Hai, Kilimo cha Mbogamboga na Matunda kwa Mwaka 2023, amesema nyenzo hizo ni muhimu sana katika kukidhi matarajio ya Sekta ya Kilimo na Uchumi, pamoja na kuimarisha afya za watu; hivyo kuna haja ya kuendelea kushirikiana na Wadau (Zanzibar Organic Initiatives) na wale wa Mbogamboga, Viungo na Matunda, ili kushuhudia matokeo ya ziada, katika kuongeza uzalishaji, kukidhi mahitaji ya ndani, mahotelini, na ikibidi hata Nje ya Zanzibar.
Amefahamisha pia kwa kusema, “jitihada hizi zinathibitishwa na utayari wa Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo, ambapo Bajeti ya Sekta ya Kilimo Zanzibar imeongezeka kwa asilimia 84, kutoka Shilingi Bilioni 53.590 kwa Mwaka 2022/23, hadi kufikia Shilingi za Tanzania Bilioni 98.716, katika mwaka huu wa 2023/2024”.
Akiorodhesha Mikakati ya ziada, katika kile alichokitaja kuwa ni kutekeleza azma njema ya Serikali kwa mustakbali wa maendeleo ya Nchi, Mheshimiwa Othman amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, imeweza kuwajumuisha Wakulima wa Unguja na Pemba, kiasi asilimia 20, katika Teknolojia ya Kilimo cha Umwagiliaji kwa Njia ya Matone (Drip Irrigation) ikihusisha aina mbalimbali za kilimo, zikiwemo Kilimo cha Mbogamboga.
“Kwa upande wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Zao la Mpunga, Teknolojia ya Uvunaji wa Maji ya Mvua, katika Mabonde zaidi ya 8, imetumika kwa kutumia Mabwawa yenye uwezo wa kukusanya zaidi ya Lita Bilioni 1 za Maji; Mabwawa hayo ni pamoja na Mlemele - Pemba, Kinyasini na Chaani - Unguja, ambayo yatakuwa na uwezo wa kudumu wa kuvuna maji kwa Kipindi cha zaidi ya Miaka 50, pindipo yakitunzwa vyema, ambapo lengo la teknolojia hizo, za upatikanaji na matumizi bora ya maji, ni kuhakikisha uzalishaji wenye tija wa mazao ya chakula, na kuondokana na kilimo cha mazoea; na hivyo kuelekea katika Kilimo cha Biashara, ili kuweza kujipatia chakula cha kutosha na kipato, kutokana na mauzo ya ziada”, amefafanua Mheshimiwa Othman.
Akigusia juu ya matumizi bora ya ardhi ndogo hapa Visiwani, kwaajili ya uzalishaji wenye tija, pamoja na kuzingatia vyema afya ya udongo katika ardhi, Mheshimiwa Othman ameeleza kwa kusema, “nimepata taarifa kwamba sasa tunavyo vifaa vya kupima afya ya udongo katika Wilaya zote za Zanzibar; hivyo, nawasihi tuvitumie vyema vifaa hivyo kivitendo, ili kufikia dhamira iliyokusudiwa; upimaji wa afya ya udongo utasaidia sana kuondokana na kilimo cha kubahatisha”.
Ameeleza azma ya Serikali kuendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika jitihada za kuongeza uzalishaji, kuendeleza kilimo, pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa Sekta Binafsi, juhudi ambazo amesema zitasaidia kuongeza kasi ya kuzalisha mazao, kuongeza tija, na hatimaye kujitosheleza kwa chakula hapa Nchini.
Akitoa angalizo juu ya ujio wa Msimu wa Mvua kubwa, Mheshimiwa Othman amesema, “naomba niwakumbushe wataalamu wetu wa sekta ya kilimo kwamba, mnao wajibu wa kuwaelimisha wakulima, namna bora ya kukabiliana na matarajio ya Mvua za Vuli zinazokuja, kulingana na maelekezo na indhari ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini, ili kuepuka athari mbaya katika kilimo, mifugo na hata kwa afya zetu”.
Pamoja na kuwahamasisha wananchi kuweka jitihada katika utaratibu wa kunywa maji kwa kiwango kinachoshauriwa na wataalamu, hatua ambayo ni muhimu kwa afya, Mheshimiwa Othman ameipongeza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa hatua ambazo inaendelea kuzichukua katika kuhakikisha kwamba malengo ya kujitosheleza kwa chakula na kukuza uchumi wa wananchi kupitia kilimo yanafikiwa.
Hata hivyo, ametoa shukrani zake za dhati kwa Washirika wa Maendeleo, Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Wajasiriamali, Wafanyabiashara na Wadau wote, kwa kuungamkono na kusaidia jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, katika matayarisho ya maonesho hayo, pamoja na kuwasihi wasichoke kufanya hivyo kwa manufaa yetu sote, na kwaajili ya Maendeleo ya Taifa.
Kabla ya hapo, Mheshimiwa Othman, ambaye katika Hafla hiyo ameambatana na Mke wake Mama Zainab Kombo Shaib, amepata fursa ya kutembelea na kukagua Mabanda ya Maonyesho ya Bidhaa za Kilimo na Ufugaji kutoka kwa Wananchi, Wizara, Taasisi, Mashirika ya Umma, Jumuiya na Asasi mbalimbali za Kiraia, hapa Nchini.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mhe. Shamatta Shaame Khamis amesema, Lengo la Maonesho hayo ni kuhimiza mapinduzi katika Sekta ya Kilimo, kwa kuelimishana mbinu bora za kilimo, ufugaji na uhifadhi wa misitu, pamoja na mazao yake.
Amesema miongoni mwa mbinu hizo ni matumizi ya teknolojia mbali mbali za umwagiliaji, sambamba na matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo na mifugo, zikiwemo mbolea, vyakula vya mifugo, malisho na mbegu bora, kwa madhumuni ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa tija zaidi, na kuwapa faida wakulima na wafugaji.
Katika Risala yenye Maudhui ya Siku hii, iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Bw Seif Shaaban Mwinyi, Wakulima wameshukuru hatua ya Serikali kuungamkono juhudi zao, sambamba na hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi kufanikisha Sehemu Kubwa ya Gharama za Maandalizi ya Maadhimisho na Maonyesho hayo, yanayogharimu takriban Shilingi za Tanzania Milioni 280, kwa kila Mwaka.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, ambayo inaadhimishwa Kimataifa, na kufikia Kilele chake ifikapo Tarehe 16 Oktoba ya kila Mwaka, kwa Mwaka huu wa 2023, ni ‘Maji ni Uhai, Maji ni Chakula, Asiachwe Mtu Nyuma’, inayolenga kuhamasisha jamii kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora; sambamba na kuongeza uelewa kwa watu wote duniani, juu ya kuyatumia maji kwa uangalifu, hasa katika zama ambazo zinashuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu, ukuaji wa uchumi, na athari za mazingira, zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ambazo zinatishia pia upatikanaji wa raslimali hizo muhimu.
Mawaziri, Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wataalamu, Jamii, Dini, Vyama vya Siasa, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wawakilishi wa Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Makundi ya Vijana wa Hamasa wa Vyama tofauti vya Siasa, Makamanda wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Wananchi na Wadau wa Kilimo kutoka ndani na nje ya visiwa vya Unguja na Pemba, wamehudhuria katika hafla hiyo.
Hafla hiyo imeambatana na harakati mbalimbali zikiwemo za Sanaa kutoka Vikundi vya Burudani, Utenzi, Wimbo Maalum kutoka Skuli ya Msingiñ Konde, Ngoma ya Msewe pamoja na Dua iliyosomwa na Sheikh Omar Hamad kutoka Ofisi ya Mufti, zote za Kisiwani Pemba.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
No comments:
Post a Comment