10 Oktoba, 2023
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyashauri
Mashirika ya umma ya
utangazaji Kusini mwa bara la Afrika kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia ya hali ya
juu kwa kuongeza vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na maendeleo na
mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya dunia.
Dk.
Mwinyi ameyasema hayo alipofungua mkutano mkuu wa 30 wa vyombo vya utangazaji
vya umma vya
nchi za Kusini mwa bara la Afrika SABA, hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndenge,
mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais
Dk. Mwinyi alisema Mashirika hayo hayana
budi kubuni, kusimamia na kutekeleza mikakati madhubuti inayopimika ili kwenda
sambamba na mabadiliko yanayojitokeza.
Alisema Afrika inashuhudia namna ya vyombo vya
utangazaji vikiwemo vyombo vya umma vya utangazaji vilivyo umuhimu kwa kutoa
taarifa zinazochangia maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na
kujenga amani, utulivu, usalama na utengamano wa Afrika.
Alisema Tanzania na nchi nyengine wanachama wa
SABA na bara zima la Afrika imekubaliana kuhakikisha vyombo vya utangazaji vya
umma kuwa vyanzo vya uhakika vya mapato ili kuhimili changamoto za kifedha na
hivyo kutimiza ipasavyo dhana ya kukuza, kulinda na kutangaza utamaduni wa Mwafrika.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo, Rais Dk. Mwinyi
aliwasihi washiriki kujadili hoja zitakazosaidia kuweka mbele maslahi ya watu
na nafasi ya Bara la Afrika katika kuandaa na kutangaza habari zinazolenga
kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kiutamadumi na utengamano wa kijamii
pamoja na kusimamia mijadala yenye mawanda mapana kwa Maslahi ya bara la Afrika
na kujenga taswira njema ya bara hilo kwa yale wanayoyatangaza ndani na nje ya
Afrika.
Pia Rais Dk. Mwinyi aliwataka washiriki wa mkutano
huo kutembelea na kujionea uzuri wa visiwa vya Zanzibar kwa kutembelea vivutio
vya utalii vilivyopo nchini ikiwemo Mji Mkongwe ambao ni mmoja wa urithi wa
dunia, Mlima Kilimanjaro, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ngorongoro, Manyara
Hata hivyo aliwasihi SABA kuendelea kubuni na kutumia
teknolojia ya kisasa ya TEHAMA, kushirikiana na kubadilishana ujuzi na uzoefu
wa huduma za utangazaji kwa umma kwa manufaa ya wanufaika wa huduma hizo
Alizungumza kwenye mkutano huo Naibu Waziri wa
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhandisi
Kundo Andrea Mathew alisema sekta ya
Habari na mawasiliano na tehama ni kielelezo muhimu cha matumisi sahihi ya
TEHAMA, aidha alieleza mashirika ya Umma yana jukumu la kuangalia vyanzo vya
kukuza maudhui sambamba na kuyataka mashirika hayo kuendelea kubadili mifumo ya
zamani (analogue) na kuja ya kidijitali ili kukuza kulinda na kuenzi maudhui ya
asili kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Naye, Waziri wa Maendeleo
ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma kwa niaba ya Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alieleza Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wadau wa bahari ili
kuendeleza sekta hiyo inayokwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na
teknolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la
Utangaji la TBC, Ayoub Rioba Chacha alisema mbali na mambo muhimu
yanayojadiliwa na mkutano huo pia ni chachu ya mabadiliko, kujifunza na
kubadilishana uzoefu baina ya mashirika ya nchi wa washiriki wa mkutano huo na
kwa kutumia teknolojia wamefanikiwa kusafirisha habari kimataifa.
Mkurugenzi wa Shirika la Utamgazaji Zanzibar,
Ramadhan Bukini alieleza mkutano huo ni muhimu kwa shirika hilo ambapo kwasasa
liko kwenye mabadiliko makubwa ya kiutendahi hasa maboresho ya usikivu wa redio
na televisheni kuendana na teknolojia ya kisasa mbali na kutoa huduma bora kwa
wananchi pia Shirika hilo limeanza kujiendesha kibiashara kwa lengo la
kujipatia mapato.
Wakati dunia inashughulikia wimbi la mapinduzi ya
nne ya viwanda inayochagizwa na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
mkutano huo wa siku tatu umepanga kujadili masuala ya TEHAMA katika ukuaji wa
uchumi wa kidijitaji kwa mataifa ya Afrika.
Huu ni mkutano wa tatu kufanyika Tanzania ambapo
wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam, wapili Arusha na huu wa Zanzibar.
IDARA
YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment