Habari za Punde

Uzinduzi wa Baraza la Manispaa Kaskazini A Unguja leo 7-10-2023

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akisalimia na Viongozi mbalimbali wa Serikali alipowasili katika Ukumbi wa Hoteli ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla leo tarehe 07.10.2023  amewahutubia Viongozi wa Chama na  Serikali pamoja na  wananchi wakati wa Hafla ya  uzinduzi wa Baraza la Manispaa ya Kaskazini "A" iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kupandishwa hadhi Baraza la Mji Kaskazini ‘’A’’ na kuwa Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ kitaibua ari na hamasa kwa Wananchi wote wa Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’ katika shughuli zao za maendeleo.

 

Akizindua Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ hafla iliyofanyika Hoteli ya Melia Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Hemed ameipongeza Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kasi kubwa ya kuimarisha utendaji kazi katika Serikali za Mitaa na kuridhia mapendekezo ya kulipandisha hadhi Baraza la Mji Kaskazini ‘’A’’ na kuwa Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

 

Amesema kuwa matarajio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Baraza hilo jipya litahakikisha huduma za kijamii zinakuwa bora na za ufanisi zaidi kwa kuwaondolea usumbufu wananchi kupata huduma hizo pamoja na kuandaa mipango bora ya kimkakati itakayotoa tija kwa Wananchi na Serikali kwa ujumla.

 

Aidha Mhe. Hemed amewasisitiza Watendaji wa Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ kusimamia vyema makusanyo kwa kutumia mifumo ya risiti za kielektroniki, kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali watu na rasilimali fedha, kuibua Miradi mbali mbali ya maendeleo, kuimrisha usafi wa mazingira na kusimamia Amani na mshikamano katika jamii.

 

Amelitaka Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ kuwa ni la mfano na litowe hamasa kwa ushindani wa kimaendeleo na kuongeza mapato Serikalini kwa kutumia fursa mbali mbali zinazopatikana katika Wilaya hiyo.

 

Ameutaka Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwa na mipango shirikishi jamii kwa kuzishirikisha Kamati za mashauriano za Shehia na Mabaraza ya wadi, Kamati za Wilaya na Mikoa ili kupata mazingatio na ushauri katika maendeleo.

 

Sambamba hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa endapo Mabaraza ya Manispaa na Miji Zanzibar yatatekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Serikali za Mitaa yataleta matokeo mazuri yenye tija na kuepusha Migogoro katika jamii.

 

Pamoja na hayo amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuridhia Baraza la Mji Kaskazini ‘’A’’ kupandishwa hadhi na kuwa Baraza la Manispaa kulikotokana na miongozo na maelekezo yake kwa watendaji wa Baraza hilo.

 

 

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Mohamed ameishukuru Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuridhia kulipandisha hadhi Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ ili kurahisisha kasi ya upatikanaji wa maendeleo na ukuwaji wa uchumi ndani ya Mkoa huo

 

Aidha amewataka watendaji wa Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ kuongeza ari, ufanisi na kasi ya utendaji wa kazi kwa kushirikiana na wananchi wa Mkoa huo  

 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud amesema Miradi mbali mbali imeimarishwa katika Mkoa huo ambayo imechangia kuongezeka kwa harakati za kimaendeleo na kukuwa kwa uchumi katika Mkoa huo sambamba na kuongezeka kwa kipato cha Mtu mmoja mmoja.

 

 

 

Mhe. Ayoub amesema Miradi mikubwa iliyomo Mkoa wa Kaskazini Unguja ni pamoja na miradi ya maji safi na salama, ujenzi wa Madarasa na Skuli za ghorofa pamoja na kutengwa kwa eneo la fungu refu kuwa ni eneo maalum la kuanikia dagaa ambalo wananchi wengi wa Mkoa huo hulitumia kwa shughuli zao za kibiashara.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kaskazini ‘’A’’ Khamis Mohamed Mohamed ameahidi kuwa Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ litaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuimarisha usafi wa mazingira na kuendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo.

 

Amesema kuwa kwa vile Wilaya a Kaskazini ‘’A’’ ni eneo la kimkakati la Serikali kiuchumi hasa kwa vivutio vya utalii watahakikisha idadi ya watalii wanaoingia katika Wilaya hiyo inazidi kuongezeka kila mwaka.

 

Aidha amesema Baraza la Manispaa Kaskazini ‘’A’’ litafanyakazi kwa kasi na ufanisi zaidi ili kuhakikisha wanapanda hadhi Zaidi kwa maslahi ya wanachi na Taifa kwa ujumla.

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

07/10/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.