SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar, imeipongeza Mamkaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini hasa kwa
mwaka wa fedha 2023/ 2024.
Pia Serikali imetoa pongezi hizo kwa
kufanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya kodi zaidi yaliyowekwa kila mwezi na
kuwa na ukuaji mzuri wa mapato ikilinganishwa na mwaka jana.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo ukumbi wa hoteli ya
Golden Tulip, Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi, kwenye sherehe za kilele
za mwezi wa Shukurani na furaha kwa walipa kodi wa Zanzibar.
Alisema, kwa kipindi cha miezi mitano (5) kutoka Julai
hadi Novemba 2023, ZRA ilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 276.063
na imefanikiwa kukusanya makusanyo halisi shilingi bilioni 288.251, sawa na
ufanisi wa asilimia 104.42. hivyo, kufanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato kwa
asilimia 21.93 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi bilioni 236.407 ya
kipindi kama hicho cha mwaka jana.
Alisema, hali hiyo
inajenga imani ya uwezekano
wa kukusanya mapato zaidi na zaidi. Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwataka wafanyakazi wa ZRA, kufanyakazi ya
ukusanyaji wa mapato kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili waepukane na vishawishi
kutoka kwa wafanyabiashara wachache wasiokuwa waadilifu.
Pia, alitoa indhari na kueleza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar haitomvumilia mfanyakazi yeyote wa ZRA na TRA Zanzibar, atayekwenda
kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma wakati wa kutekeleza majukumu yake ya kila
siku. Alionya, mfanyakazi yeyote atakaebainika kukwepesha mapato ya Serikali, hatua
kali za kiutumishi na kijinai zitachukuliwa dhidi yake.
Katika hali nyengine Rais Dk. Mwinyi
aliwaahidi watumishi wa ZRA kuwa Serikali itaendelea kuyaangalia maslahi yao
kama walivyoangaliwa wafanyakazi wengine wa Serikali ili kuongeza hamasa ya ukusanyaji
wa mapato pamoja na kuiwezesha ZRA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Hivyo, Dk. Mwinyi aliziagiza Wizara ya
Nchi Ofisi ya Rais Utumishi washirikiane na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha
na Mipango, kukamilisha marekebisho stahiki ya mishahara ya watumishi wa ZRA,
ili wapate faraja na waendelee na ufanisi katika kazi zao.
Kwa upande wa wafanyabiashara wote waliopo Zanzibar na wanaokuja kuwekeza, Dk. Mwinyi aliwahakikishia
kwamba Serikali imeimarisha mfumo wa kodi iliyo rafiki itakayorahisisha
biashara kwa kuimarisha mfumo
wa kodi ulio sawa kwa kila mfanyabiashara.
“Hakuna atakayependelewa wala kuonewa.
Tutaendelea kuimarisha mfumo wa kodi ulio rahisi kuutumia (convenient) kwa
kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya kidigitali na kuwafikia walipakodi wengi zaidi
kwa kuimarisha Ofisi za kodi” Dk. Mwinyi, aliwahakikikisha wafanyabiashara hao.
Vile vile Rais Dk. Mwinyi, aliitaka mikoa
na wilaya zote nchini kuendelea kuimarisha mfumo wa kodi unaotabirika (certainty) kwa kuendelea kutoa elimu
ya kodi ili kila mfanyabiashara ajue aina ya kodi anayostahiki kulipa kwa
wakati husika.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum,
akizungumza kwenye hafla hiyo alisema, kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 60
ya Mapinduzi ya Zanzibar Maendeleo makubwa yamefikiwa kutokanana ukusanyaji
mzuri wa mapato yaliyosaidia kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo.
Alisema Maendeleo hayahitaji vikwazo, ufinyu wa Maendeleo
unatokana na kukosa maono, alieleza Zanzibar imejifunza utayari kutoka kwa Rais
Dk. Mwinyi wakitafakari zaidi bila kuweka vikwanzo vya Maendeleo.
Alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa nchini ni
jitihada za Mhe. Rais Dk. Mwinyi kushajihisha ulipaji bora wa kodi za
kielektroniki.
Naye, Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya ZRA, Prof. Hemed Rashid
Hikmany, alieleza miongozi mwa majukumu ya bodi hiyo ni kuhakikisha
wanafanyakazi wanafanyakazi kwa mujibu wa sheria zilizopo na kuhakikisha walipa
kodi wanalipa kwa hiari, kuhakikisha wanafanyakazi kwa ukaribu na weledi ili
kufikia malengo ya Serikali ya ukusanyaji bora wa mapato.
Kamishna Mkuu wa ZRA, Yussuf Juma Mwenda naye alieleza mafanikio
makubwa yaliyofikiwa na ZRA ikiwemo kushajihisha walipakodi kwa ufanisi kupitia
mfumo wa kisasa wa ZIDRAS unaowarahisishia walipakodi wa aina zote, wakubwa,
wakati hadi wadogo kulipakodi na kurejesha marejesho ya kodi (returns) kwa
wakati kupitia teknolojia ya kisasa.
Alisema, ZRA pia imefanikiwa kutoka makusanyo ya Shilingi bilioni
565 kwa mwaka jana ikilinganishwa na bilioni 374 za kipindi kilichopita.
Pia alieleza ZRA imeanza kuchukuakoti za majengo ya ghorofa
ikiwemo mahoteli ambao wamekuwa na mwitikio mkubwa kwa serikali, alisema nyumba
ndogo hazihusiki na kodi hiyo.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment