Habari za Punde

UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE (JNHPP) WAFIKIA ASILIMIA 94.78

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.  Dkt. Doto Biteko ( Wa Pili kushoto) na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (wa tatu kushoto) wakikagua Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP),
Tarehe 28 Desemba, 2023 mkoani Pwani.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Mhe.  Dkt. Doto Biteko  ( wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (wa Pili kulia)  wakipata maelezo ya Maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere(JNHPP), Tarehe 28 Desemba, 2023 mkoani Pwani.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.  Dkt. Doto Bitekoakizungumza  na Timu ya Wataalam ya Usimamizi wa Mradi kutoka Ofisi ya Rais( Ikulu),Watekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wataalam
wengine wanaohusika na Mradi huo, kabla ya wakati wa ziara ya kukagua Tarehe 28 Desemba, 2023 mkoani Pwani.

*Mashine Mbili za Megawati 47O zimeshafungwa, majaribio yameanza

*Ujazo wa maji watosha kuanza kuzalisha umeme
Dkt. Biteko asema kipaumbele ni upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema
kuwa, utekelezaji wa  mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP)
utakaozalisha megawati 2,115 kwa sasa umefikia asilimia 94.78 huku
mashine mbili za kuzalisha umeme zikiwa tayari zimeshafungwa kwa ajili
ya kuanza kuzalisha umeme.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 28 Desemba 2023 wakati alipofanya
ziara ya kukagua mradi huo wilayani Rufiji akiwa ameambatana na Naibu
Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati aliyoteua
Rais ya ufuatiliaji mradi wa JNHPP, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi
Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na wataalam kutoka
Wizara ya Nishati na TANESCO.

" Hatua iliyopigwa ya utekelezaji wa mradi huu kila mtu ameona kuwa ni
kubwa kwenye hatua zote, mfano kwenye ujazaji maji wa bwawa la
kuzalisha umeme, maji yamejaa kwa kiwango ambacho yanaruhusu kuzalisha
umeme, pia ufungaji wa mashine ambazo zitatumika kuzalisha umeme,
nafurahi kusema kuwa mashine mbili zimeshafungwa ambazo ni mashine
namba Tisa na namba Nane na tunaamini kwamba mashine nyingine
zitaendelea kufungwa kadri muda  unavyoenda ili kupata megawati zote
2,115." Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, kufungwa kwa mashine hizo mbili kunatoa
matumaini ya kutekeleza agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
la kupunguza changamoto za umeme nchini ndani ya miezi Sita ambapo
sasa imebaki miezi mitatu ya utekelezaji wa agizo hilo kwani mashine
hizo zitazalisha megawati 470 na kuingizwa katika gridi ya Taifa ili
kuongeza kiwango cha umeme.

Ameeleza kuwa,  mashine namba Tisa itakapofika tarehe 2 Januari
majaribio ya kwanza yajulikanayo kama dry testing yatakuwa
yamekamilika na ifikapo mwezi Februari  tarehe 19 majaribo ya pili
yajulikanayo kama wet testing yatakuwa yamekamilika tayari kwa kuanza
kuzalisha umeme na kwa mashine namba Nane matarajio ni kuwa, na
yenyewe majaribio yakamilike mwezi Februari 2024.

Kuhusu ujazaji maji amesema kuwa, ujazo wa maji katika Bwawa la
kuzalisha umeme ni mita za ujazo 166.65 juu ya usawa wa bahari ambayo
yanatosheleza kuanza kuzalisha umeme kwani kima cha maji ambacho
kinaweza kuzalisha umeme ni mita za ujazo163.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, ni kweli kuna
changamoto ya umeme hivyo kipaumbele kwa sasa ni kujikita katika
kupata umeme wa uhakika na wananchi wana haki ya kujua hatua
mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ili kuondoa changamoto hiyo.

Ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mabwawa ya
uzalishaji umeme, Dkt. Biteko ameelekeza TANESCO kuwa sehemu ya
mkakati ya utunzaji mazingira, kwani baadhi ya watu wanachepusha mito
na kuharibu mazingira hali ambayo inapelekea hadi umeme kutozalishwa
wa kutosha na anayelaumiwa ni TANESCO hivyo amelitaka Shirika hilo
kutenga fedha za kutosha ila kila mdau anayehusika katika usimamizi wa
mazingira ahusishwe.

Pamoja na kupongeza wataalam kwa kazi nzuri ya ujenzi mradi wa JNHPP,
amewataka kwenda kwa kasi zaidi kwani takriban watu milioni 63 nchini
wanaitegemea TANESCO kupata umeme wa uhakika.

Vilevile, Dkt. Biteko amemtaka Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati
kusimamia suala la TANESCO, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (
TPDC)  na Idara  ya Sera na Mipango, Wizara ya Nishati, kuja na mpango
wa miaka 20 au 30 ijayo wa upatikanaji nishati kiwemo umeme kwani
mahitaji yanazidi kuongezeka na Wizara ya Viwanda na Biashara
ishirikishwe ili kuwa na mipango thabiti ya upatikanaji na usambazaji
umeme ikiwemo kwenye viwanda ambavyo vinazidi kuongezeka.

Gharama za utekelezaji mradi wa JNHPP ni Trilioni 6.5 na Serikali
imeshamlipa mkandarasi kampuni ya JV Elsewedy na Arab Contractors
shilingi Trilioni 5.76 ambayo ni sawa na asilimia 87.83.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.