Habari za Punde

Wakulima wa Kaskazini Kunufaika na Mikopo ya Benki ya TADB

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akikata utepe wakati wa uzinduzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Kaskazini mkoani Arusha. Wa tatu kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TADB, Bw. Ishmael Kasekwa na wa nne kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege.

Na. Peter Haule, WF, Arusha

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameiagiza Menejimenti ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iweke masharti nafuu ya mikopo ili kuwezesha wakulima, wavuvi na wafugaji kupata mikopo hiyo kwa wakati na kwa gharama nafuu.

 

Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo jijini Arusha wakati akizinduzi Ofisi ya Kanda ya Kaskazini ya Benki ya hiyo itakayohudumia mikoa ya ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.

 

” Aidha Maafisa Biashara wa Benki wekeni utaratibu wa kuwatembelea wakulima na kuona maendeleo ya miradi yao mara kwa mara, kwa kufanya hivyo mtasimamia vizuri fedha zitakazotolewa na kuweza kuleta marejesho na faida kwa Benki”, alieleza Dkt. Nchemba.

 

Vilevile ameiagiza Menejimenti ya Benki hiyo kuweka utaratibu wa kujitangaza na kutangaza fursa za mikopo wanayoitoa kwa wakulima na wafugaji ili waweze kuzitumia kwa wakati na kwa tija, pia kutoa elimu kuhusu usimamizi ya mipoko kwa wakulima watakaokopeshwa.

 

Mhe. Dkt. Nchemba alitoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga kuchangamkia fursa ya uwepo wa Ofisi ya Kanda ya Kaskazini ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Arusha, kupata uelewa  zaidi wa utaratibu wa kupata mikopo ya pembejeo bora, zana za kisasa za kilimo ili wapate tija kupitia kilimo.

 

Mhe. Dkt. Nchemba aliwataka wanufaika wote wa mikopo kutoka TADB katika Kanda hiyo, wafanye matumizi sahihi ya fedha watakazokopeshwa ili kuendeleza miradi ambayo imeombewa fedha hizo katika mchanganuo wa maombi ya mikopo hiyo.

 

Akizungumzia kuhusu jitihada za Serikali katika kukuza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, Dkt. Nchemba, alisema kuwa imeongeza bajeti Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambapo katika bajeti ya mwaka 2023/2024, kupitia Wizara ya Kilimo, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 970.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 29.2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2022/2023.

 

Alisema kuwa Kwa upande wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 292.5 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo sekta ya Mifugo imetengewa shilingi bilioni 112.1 na Sekta ya Uvuvi imepangiwa kutumia shilingi bilioni 180.5. 

 

“Matarajio ya Serikali ni kwamba jumla ya shilingi trilioni 1.2, ambazo tuliziidhinisha katika Wizara hizo mbili zitakwenda kuchochea kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa, pamoja na kuongeza fursa za ajira na kipato kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo tatu na kuongeza mchango wao kwenye Pato la Taifa’’, alisema Dkt. Nchemba

 

Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo, sekta ya kilimo inatoa ajira kwa wastani wa asilimia 75 ya Watanzania wote, inachangia asilimia 100 ya chakula kinachozalishwa nchini na zaidi ya asilimia 65 ya malighafi viwandani na inachangia robo ya Pato la Taifa na robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TADB, Bw. Ishmael Kasekwa, alisema kuwa ili kuweza kuleta matokeo chanya, Bodi ya Wakurugenzi wa TADB imeisimamia kwa weledi na uzalendo Benki ya TADB ili kuhakikisha malengo kusudiwa kwa Serikali na wakulima yanafikiwa.

 

Alisema kuwa licha ya kuwa TADB ni changa katika soko la biashara ya mabenki, kwa muda mfupi imeanza kuona ukuaji endelevu na faida ambapo katika mwaka 2021, ilipata faida ghafi ya shilingi bilioni 16 na mwaka 2022 ilipata faida ya shilingi bilioni 15.6

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, alisema kuwa TADB ina Ofisi saba ambazo zipo Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya, Kanda ya Mashariki mkoani Dar es salaam, Kanda ya Magharibi mkoani Tabora, Kanda ya Kati mkoani Dodoma, Kanda ya Kusini mkoani Mtwara na sasa Kanda ya Kaskazini yenye ofisi Jijini Arusha.

 

Alisema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo mwaka 2015 kwa lengo la kuchangia utoshelevu wa chakula na kuchagiza mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara.

 

Bw. Nyabundege alisema katika kutekeleza suala hilo, Serikali iliielekeza Benki hiyo kutoa mikopo kwa wakuliwa wadogo, wa kati na wakubwa katika mnyororo mzima wa thamani hivyo kuwezesha upatikanaji wa mitaji na kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo.

 

Akizungumza kuhusu Mtaji wa Benki hiyo, Bw. Nyabundege alisema, Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani TADB ilikuwa na mtaji wa shilingi bilioni 60, lakini Serikali iliongeza mtaji wa shilingi bilioni 208, mwaka 2021 na hivi karibuni Serikali imetafuta mtaji mwingine wa takribani shilingi bilioni 165 sawa na dola milioni 66 kutoka Benki ya Maendelo ya Africa (AfDB).

 

Alisema kuwa hadi kufikia Novemba, 2023, katika Kanda ya Kaskazini, TADB imewezesha wakulima na wafugaji kwa kutoa mikopo wa shilingi bilioni 18.3 kwa Mkoa wa Tanga, shilingi bilioni 7.9 Mkoa wa Arusha, shilingi bilioni 3.2 Mkoa wa Kilimanjaro na shilingi bilioni 3.1 kwa mkoa wa Manyara.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili kushoto) akifungua rasmi Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Kanda ya Kaskazini mkoani Arusha. Wa pili kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TADB, Bw. Ishmael Kasekwa na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akieleza umuhimu wa Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Kanda ya Kaskazini mkoani Arusha, katika kuendeleza Sekta ya Kilimo na Uvuvi. 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akitoa rai kwa wakulima Kanda ya Kaskazini kutumia fursa ya uwepo wa Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Kaskazini mkoani Arusha, kukopa ili kuweza kupata pembejeo bora za kilimo.
Viongozi na wadau mbalimbali wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Kaskazini, mkoani Arusha

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TADB, Bw. Ishmael Kasekwa (wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Benki hiyo na watumishi baada ya kuzinduliwa kwa Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Kanda ya Kaskazini mkoani Arusha.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha)


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.