Habari za Punde

Wanawakev Watakiwa Kusomea Ubaharia Kukuza Uchumi

Mkuu wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) dkt. Tumaini Gurumo   akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa zinazopatikana katika chuo hicho walipotembelea banda la DMI katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika  kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.
Mkuu wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) dkt. Tumaini Gurumo akielezea kuhusiana na fani zinazosomeshwa katika chuo hicho  alipotembelewa na waandishi wa habari  katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika  kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.

Na Fauzia Mussa , Maelezo Zanzibar.

Mkuu wa chuo cha bahari Dar-es-salaam (DMI) dkt. Tumaini Gurumo  amewataka wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao wakike kusomea fani za ubaharia ili kuweza kuzifikia fursa zitokanazo na uchumi wa buluu na kujiletea maendeleo.

Wito huo ameutoa wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari walipotembelea banda la chuo hicho katika maonesho ya 10 ya biashara yanayoendelea katika  kituo cha biashara Nyamanzi Zanzibar.

Alisema ili kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu kwa vitendo  ipo haja kwa vijana  kuendelea kujiunga na chuo hicho bila kujali jinsia ili kupata mafunzo yatakayowawezesha  kuingia katika utekelezaji wa dhana hiyo,kwani bila rasilimali watu wenye weledi lengo la uchumi wa buluu halitafikiwa.

Amesema dhana ya uchumi wa buluu imeenda kuongeza ari na kasi  kwa wazanzibar kujiunga  kwa wingi siku hadi siku katika chuo hicho, na kusema kuwa kutokana na mwamko huo  chuo kina mpango wa kuanzisha tawi kisiwani pemba ili kuhakikisha Tanzania nzima inaunufaika na huduma za chuo hicho.

“mwamko wa wazanzibar kujiunga na chuo hichi ni mkubwa sana kwasasa tuna mpango wa kutafuta eneo pemba ili tuweke tawi la chuo chetu  kwa lengo la kusogeza huduma kisiwani humo,tusipofanya hivyo tutakua tunakaribisha wageni kujakufanya kazi katika maeneo yetu na kupelekea uchumi tuliokusudia urudi nyumbani kwenda kwa wageni” alifahamisha dkt. Tumaini

Amesema ili nchi ipate maendeleo si vyema kuwawekea wasichana   mipaka ya kusomea fani fulani kwani nafasi za ajira zilizopo maelini hazichagui jinsia.

Alieleza kuwa  kwa sasa mwamko wa wanawake kusomea fani hiyo ni mdogo hivyo alitumia fursa hiyo kushajihisha wazazi na walezi  kuwapa nafasi wasichana kusomea fani hiyo kwa maslahi yao  binafsi na taifa kwa ujumla.

“tuwaache vijana wasomee fani wanazozipenda ,hakuna kitu kizuri kama mtu kufanya kazi anayoipenda ,wanawake wana haki ya kusomea ubaharia pia na hata sheria zinatoa haki sawa na maslahi kati ya wanawake na wanaume”alifahamisha mkuu huyo.

Amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wazanzibar kwa ujumla wamekuwa  na mwamko mkubwa wa kusomea fani ya ubaharia chuoni hapo  licha ya kuwa chuo chenyewe kipo Dar-es-salaam.

Akizungumzia  mafanikio ya miaka 60 ya mampinduzi katika chuo hicho dkt. Tumaini alisema chuo  kimefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka  wanafunzi 12 kwa mwaka 1978 hadi kufikia kuwa na   zaidi ya wanawafunzi elfu 4 kwa mwaka 2023-2024.

Aidha alifahamisha kuwa chuo hicho  kimekua kikitengeneza rasilimali watu zinazoweza kunufaisha ukanda mzima wa Tanzania na nje ya Tanzania pamoja na kufanikiwa kufanya tafiti za bahari ili kuweza kufanya vizuri katika dhana ya uchumi wa buluu.

“Ili tuweze kuanya vizuri katika uchumi wa buluu ni lazima tufanye tafiti kuweza kutathmini ni upande gani tuende zaidi ,kama ni uvuvi wa aina gani utaleta tija zaidi” alisema dkt. Tumaini.

Licha ya mafanikio hayo dkt. Tumaini alisema kuwa chuo kinakabiliwa na  uhaba  wa walimu mabaharia wenye sifa zinazokubalika  kulingana na uhitaji wa wingi wa wanafunzi wanaongezeka kusajiliwa siku hadi siku.

Vilevile wanafunzi wamekuwa wakikosa nafasi za kushiriki mafunzo kivitendo katika meli zinazosafiri kutoka nchi moja kwenda nyengine,hivyo aliziomba taasisi za usimamizi wa meli za serikali na binafsi kusaidia wanafunzi wengi kupata nafasi za mafunzo melini ili kurahisisha upatikanaji wa ajira za nje na ndani ya nchi kwa vijana hao.

Awali alifahamisha kuwa  lengo la kushiriki katika maonesho hayo ni kutangaza shuguli zinazofanya na chuo hicho ambapo alisema ni pamoja na kutoa elimu na mafunzo ya mabaharia na masuala yanayohusiana na bahari kama uchimbaji wa gesi,utunzaji wa mzingira na usalama baharini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.