Habari za Punde

Kusini na Kaskazini Unguja Wafikiwa na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma

Mkuu wa kitengo cha uhusiano na elimu kwa umma tume ya maadili ya viongozi wa umma Halima Jumbe Said akijenga uwelewa kwa wakaazi wa Shehia ya Kitope,Matetema na Shehia ya Kwagube Mkoa wa kaskazini Unguja .

Na Fauzia Mussa. Maelezo. 28.02.2024.

Wananchi wa Mkoa wa kusini na Kaskazini Unguja wameiomba Tume ya maadili ya viongozi wa umma kutoa elimu mara kwa mara ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa tume hiyo Nchini.

Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati maafisa wa Tume hiyo walipofanya ziara ya kutoa elimu kwa wananchi wa Mikoa hiyo.

Wamesema uelewa kwa jamii, juu ya majukumu ya Tume hiyo bado ni mdogo jambo ambalo linapelekea kuchelewa kufikia malengo mazuri yaliyopangwa na Serikali.

Aidha wamesema endapo jamii itakua na uelewa wa kutosha juu ya Tume ya maadili ya Viongozi wa umma, itaweza kuwafahamu viongozi wanaokiuka maadili pamoja na kujengeka ujasiri wa kutoa taarifa za viongozi hao sehemu husika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Mbali na hayo Wananchi hao wameiomba Tume hiyo, kuimarisha ulinzi na usalama kwa wanaotoa taarifa pamoja  na kutoa motisha kwa wananchi ili jamii iendelee kuwafichua viongozi wanaokwenda kinyume na Maadili.

Hata hivyo Wananchi hao, wamewashauri Wazazi na Walezi kushirikiana katika malezi ya watoto kwa kufuata misingi ya maadili ili kuepusha kuwa na viongozi wasio na maadili hapo baadae.

Mapema Mkuu wa kitengo cha uhusiano na elimu kwa umma katika Tume ya maadili ya viongozi wa umma Halima Jumbe Saidi amesema Tume hiyo inawajibu wa kutunza siri zinazotolewa na Wananchi sambamba na kufanyakazi kwa ushirikiano  kati ya tume hiyo  na Wananchi ili kuhakikisha haki zinapatikana.

Halkadhalika amesema tume itendela  kutoa elimu ili jamii ipate uelewa na kutoa taarifa za viongozi wanaokwenda kinyume na maadili kwani miongoni mwa majukumu mengine ya tume hiyo ni kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kupokea malalamiko ya viongozi wanaokwenda kinyume na maadili .

“ Serikali imeweka taasisi mbalimbali za kutoa elimu ya maadili ikiwemo tume hii , Ofisi ya mufti , na Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto ili kuhakikisha jamii yote inaishi kimaadili mema yanayokubalika katika jamii.”alisema Bi Halima.

Hata hivyo aliwasisitiza wananchi kufika Ofisi za tume ya maadili ya viongozi wa umma kupeleleka malalamiko dhidi ya viongozi wanaowatuhumu kufanya ubadhirifu na kuahidi kuwa tume hiyo, itaendelea kusikiliza madai ya mwanachi yoyote dhidi ya kiongozi anakwenda kinyume na maadili kwa usiri.

Kwa upande wake Afisa kutoka tume hiyo Habib Said Mohammed amesema kuna baadhi ya viongozi wanadaiwa wanajihusisha na vitendo vya rushwa, kutelekeza familia zao, kutumia mali za umma kwa maslahi yao binafsi na kutumia madaraka vibaya jambo ambalo kinyume na maadili ya Tume hiyo.

Akitaja adhabu kwa viongozi watakaobainika kwenda kinyume na maadili  amesema kuwa ni pamoja na kusimamishwa au kufukuzwa kazi, kukatwa mshahara na kushauriwa kujiuzulu kulingana na kosa alilofanya.

Tume ya maadili ya viongozi wa umma imetoa elimu katika shehia mbalimbali za Mkoa wa Kusini Unguja ikiwemo Shehia ya Kijini, Nganani na Kiongoni na kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ni pamoja na Shehia ya Kitope, Matetema na Kwagube.

Afisa kutoka tume ya maadili ya viongozi wa umma Habib Said Mohammed akisikiliza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa mkoa wa kaskazini Unguja wakati wakitoa elimu ya tume hiyo huko Skuli ya Kitope.
Afisa kutoka tume ya maadili ya viongozi wa umma Habib Said Mohammed akisikiliza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa mkoa wa kaskazini Unguja wakati wakitoa elimu ya tume hiyo huko Skuli ya Kitope.
Afisa kutoka tume ya maadili ya viongozi wa umma akigawa vipeperushi vya tume ya maadili wakati wakitoa elimu ya tume hiyo kwa wanachi wa mkoa wa Kusini Unguja.
Mwananchi wa shehia ya Kijini Nachoum Mussa Haji akichangia wakati wakipatiwa elimu ya tume ya maadili huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwanachi wa Shehia ya Kitope Issa Ali akichangia wakati wakipatiwa elimu ya Tume ya maadili wa viongozi wa umma huko Skuli ya Kitope Mkoa wa kaskazini Unguja .

Afisa kutoka tume ya maadili ya viongozi wa umma Habib Said Mohammed akisikiliza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi  wakati wakitoa elimu ya tume hiyo huko Koba mkoa wa Kusini Unguja.

Picha na Fauzia Mussa --Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.