Habari za Punde

Waziri Mhe.Mhagama Akabidhi Magari na Pikipiki Zenye Thamani ya Zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili kwa Watekelezaji wa Programu ya AFDP


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi (Magari na pikipiki) kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)  tarehe 12 Machi, 2024 iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi hizo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma

NA; MWANDISHI WETU – DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili za kitanzania kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)  Mapema leo tarehe 12 Machi, 2024 katika viwanja vya Ofisi hizo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma.

Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni Magari, pikipikiza miguu miwili na mitatu (guta) kwa wawakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Wizara ya Kilimo, Wakala wa Mbegu (ASA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Taasisi za Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) na Mratibu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Waziri Mhagama alieleza kuwa upatikanaji wa vifaa vinavyonunuliwa kupitia Programu hiyo ikiwemo magari na pikipiki, ni vitendea kazi muhimu katika utekelezaji wa Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 bila ya kusahau  Ununuzi wa meli nane (8) kwa ajili ya uvuvi katika bahari kuu na kuendeleza ukuzaji viumbe maji, na kilimo cha  Mwani.

“Vilevile, Programu hii inalenga kuongeza uzalishaji, tija na faida katika shughuli za wakulima kwa kuendeleza shughuli za ugunduzi na uzalishaji wa mbegu bora na kuhamasisha kilimo cha mazao lishe (nutritional sensitive) ili kupunguza udumavu.” Alifafanua Waziri Mhagama

Aliendelea kusema kuwa Programu hiyo inaenda kuleta mabadiliko makubwa kwenye uzalishaji na uendelezaji wa biashara kwa kuzingatia mazingira halisi yaliyopo na hasa uboreshaji wa uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo, mahindi, alizeti, maharage na mimea jamii ya kunde pamoja na uboreshaji wa sekta ya uvuvi, mifugo na ufugaji wa viumbe maji kwa lengo la kuwaendeleza na kuwawezesha akina mama na vijana wa kitanzania kunufaika zaidi na sekta hizo mbili.

Akizungumza kwa Niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar) Mheshimiwa Hamza Hassan Juma alisema matunda ya mafanikio haya ni matokeo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mw. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekhe Abeid Amani Karume takribani miaka sitini iliyopita, “kwenye zoezi hili kuna kipengele cha ununuzi wa meli za uvuvi ambazo tutazipata sisi kutokana na faida ya Muungano wetu.” Alibainisha

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde alisema vifaa hivyo vitaenda kuchochea kasi ya utekelezaji katika sekta ya kilimo hasa katika shughuli mbalimbali zilizopangwa katika utekelejazi wa program hiyo na kutoa rai kwa taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo zinahakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa  malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kufikia malengo ya Programu.

Akiongea kwa Niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Riziki Shemdoe alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongonzwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali katika kuendeleza sekta ya Uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi ya bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko ambapo Meli za uvuvi za kibiashara zitakazonunuliwa kutokana na program ya (AFDP) zitatia nanga katika bandari hiyo.

Awali akiongea katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa alisema Lengo kubwa la Progrmamu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)kuchangia katika mfumo Jumuishi ya chakula ili kuboresha Maisha, usalama wa chakula,lishe na ustahimilivu kwa kuongeza uzalishaji pia kuongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na biashara ya baadhi ya mazao uvuvi na ufugaji wa viumbemaji na jumla ya kaya laki 260 zinatarajiwa kufikiwa katika program hii katika mikoa 11.

Picha ikionesha baadhi ya vifaa vilivyoabidhiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)  Mapema leo Tarehe 12 Machi katika halfa ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi hizo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma.
Picha ikionesha baadhi ya vifaa vilivyoabidhiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)  Mapema leo Tarehe 12 Machi katika halfa ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi hizo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.