Habari za Punde

Serikali Kwa Kushirikiana na Wadau Waendesha Mafunzo ya Utambuzi wa Noti

Na WMJJWM-Bukombe Geita

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kuwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMIVITA) na Benki Kuu ya Tanzania imeendesha mafunzo ya utambuzi wa noti kwa Watu wenye Ulemavu hususani Viziwi.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis leo Mei 10, 2024 Wilayani Bukombe mkoani Geita, amesema Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye Ulemavu katika masuala ya elimu, uwezeshaji kiuchumi, afya, ajira, nyenzo za kujimudu pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuwawezesha na kuwaunganisha na fursa zilizopo katika jamii.

Ameongeza Serikali inatambua kuwa watu wenye Ulemavu wakiwemo Viziwi bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha wengi wao kutofikia malengo yao. Kutokana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali sambamba na kutekeleza matakwa ya Sheria ya watu wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 - 2025. 

"Nitumie fursa hii kuwashukuru wadau wa maendeleo mlioshiriki kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watu wenye Ulemavu na ni dhahiri mmekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazolenga kumuwezesha kila mwananchi na hali yake kupata huduma stahiki na kwa wakati." amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.

Aidha amelitaka kundi hilo kuchangamkia fursa za fedha zinazotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inayotoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia benki ya NMB kwa wafanyabiashara wadogo ambapo Mheshimiwa Rais ametoa bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo.

 "Fikeni Halmashauri, hususani Ofisi za Maendeleo ya Jamii ili waweze kuwapa utaratibu wa kupata mikopo hiyo.Pia, ninawasihi mjisajili na kupata vitambulisho vya wajasiriamali wadogo (Maarufu MACHINGA) mara vitakapoanza kutolewa ili muweze kukopesheka katika taasisi za fedha na Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani katika mikopo ya 10% (4-4-2) ambayo Mheshimiwa Rais ameelekeza ianze kutolewa kuanzia mwaka wa fedha 2024/25 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu." amesema Naibu Waziri Mwanaidi 

Kwa upande wake Katibu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMIVITA)  Wilaya ya Bukombe Kevin Nyema ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo muhimu yatakayowasaidia kutambua noti wakati wa shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na kuwapa fursa zaidi ya kushiriki pia katika shughuli hizo kikamilifu.

"Asante sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutujali sisi watu wenye ulemavu, wadau mbalimbali wakiwemo Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwezesha mafunzo haya" alisisitiza Nyema

Mafunzo ya utambuzi wa noti kwa watu wenye ulemavu husani viziwi yanaratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuzingatia miongoni na kanuni mbalimbali za fedha nchini kwa lengo la kuwapa uwezo kundi hilo kukabiliana na changamoto za kifedha ikiwemo utapeli unaohusisha utoaji na upokeaji wa pesa zisizo halali. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.