Habari za Punde

UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI SKULI YA SEKONDARI - MAKUNDUCHI





Makamo wa Pili wa Raiswa Zanzibar amesema haridhishwi na mwenendo wa Utendaji kazi wa Kampuni ya FUCHS CONTRACTION ianayojenga Skuli ya Sekondari ya Mkunduchi kwa kusababisha kuchelewa kumalizika kwa wakati kwa Mradi huo na kuwataka wakandarasi kuutumia muda wa makubaliano uliopangwa kwa  kumaliza Ujenzi ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa skuli ya Sekondari ya makunduchi  Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar amesema serikali imeamua kuwapa wakandarasi wazawa kujenga majengo ya Skuli za ghorofa ili kuweza kuwasaidia katika utendaji kazi hivyo ni lazima kuthamini juhudi za serikali katika kuwalete maendeleo wananchi sambamba na kuwatatulia changamoto zote zinazowakabili ikiwemo upatikanaji wa mazingira bora ya kusomea.

Mhe. Hemed  amesema kukamilika kwa  ujenzi wa Skuli hiyo utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kwa kukosekana mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ikowemo kufuata elimu ya Sekondari masafa marefu, hivyo ni wajibu wa wakanadarasi kufanya kazi wa bidii ili kuendana na makubaliano ya mkataba uliopo  baina yao na serikali.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia iIani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 Sera na Mikakati imeelekeza kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa elimu nchini ikiwemo kujenga skuli mpya za kisasa kuanzia Maandlaizi, Msingi na Sekondari ili kuendana na kasi ya ongezeko la idadi ya wanafunzi mashuleni.

Akizungumzia suala  Ajira  Mhe. Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa ameshauagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu kutoa kipaombele cha ajira kwa vijana wazawa wa Mkoa husika uliopitiwana Miradi ya Elimu ili kupunguza changamoto ya kuajiri walimu wanaotoka masafa ya mbali na skuli na kusababisha kuzorotesha kwa ufanisi maskulini.

Mhe. Hemed ameikumbusha jamii kuwa ni jukumu la kila mtu kuilinda miundombinu ya elimu ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwataka walimu kuendelea kusomesha kwa bidii ili kuzidi kupata ufaulu mzuri kwa wanafunzi na kuzalisha wataalamu wengi wanaohitajika katika Taifa.

Sambamba na hayo  amewaasa wanafunzi nchini kuitumia na kuitunza vyema miundombinu ya elimu kwa kujifunza ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na iweze kutumika kwa vizazi vya sasa na baadae.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed Mussa amesema nia ya Serikali na Wizara ya Elimu ni kuhakikisha wanawaajiri waalimu wazawa wanaoishi katika maeneo yanayojengwa maskuli ili kuzidisha ufaulu kwa wanafunzi na kutengeneza mazingira rafiki ya kujisomea na kufundishia kwa walimu na wanafunzi.

Amesema Asilimia Hamsini (50) ya  Bajeti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2024-2025 imeelekezwa katika miradi ya Elimu sambamba na kuboresha miundombinu ya elimu lengo ni kuondoa kabisa devision Zero Zanzibar.

Waziri Lela amesema ni vyema wakandarasi wa ujenzi wa skuli hio kutoka kampuni ya Fuchs Contraction  kuzitumia changamoto walizo nazo kuwa ni Fursa kwao ili kuweza kukamiloisha ujenzi huo kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa ili kuweza kuishawishi seriakli kuwapatia miradi mengine inapotokezea.

Sambamba na hayo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali amemuomba Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwaagiza Watendaji wa Tume ya Utumishi Serikalini kuiangalia vyema mifumo ya ajira ambayo imekuwa ikileta malalamiko mengi kwa wananchi ambao wameshamaliza kusoma na wengine kujitolea katika maskuli mbali mbali Unguja na Pemba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amesema Mkoa wake umenufaika na Miradi mingi  ya maendeleo hasa katika Sekta ya Elimu jambo lililochangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika Mkoa huo.

Ayoub ameiomba Serikali kupitia Wizara ya elimu kusimamia Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Makunduchi ili uweza kumalizika kwa haraka na kuondoa changamoto ya wanafunzi kufuata skuli masafa ya mbali hasa katika kipindi hiki ambacho vitendo vya udhalilishaji vinaongezeka siku hadi siku,  Sambamba na kuishauri wizara kuajiri walimu wanaotoka sehemu husika ili kuondoa changamoto zote zinazojitokaza.

Ujenzi wa skuli ya Sekondari ya Makunduchi utakapokamilika utakuwa na madarasa 42 ya kusomea, Maabara tatu(3), Maktaba mija(1), chumba kimoja cha Komputer, ofisi za walimu na vyoo 31 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 6 hadi kukamilika kwake.

 

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)

Tarehe   25.05.2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.