Habari za Punde

Warsha ya Kitaifa Kujadili Shabaha za Kuondoa Uharibifu wa Ardhi na Mbinu Shirikishi ya Tathmini ya Ardhi (ILAM) Yafanyika Morogoro

Wataalamu na wadau wa sekta mbalimbali nchini walishiriki katika warsha ya siku mbili kwa ajili ya wajumbe wa Kitaifa wa Shabaha za Kuondoa Uharibifu wa Ardhi (Land Degradation Neutrality National Working Group – LDN WG) sambamba na mafunzo ya Mbinu Shirikishi za Tathmini ya Ardhi (Integrated Land Assessment Methodology – ILAM).

Akifungua warsha hiyo iliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame Tanzania jijini Morogoro, Dkt. Deogratius Paulo, Mkurugenzi Msaidizi-Ofisi ya Makamu wa Rais, aliwataka wataalamu na wadau hao kuhakikisha kuwa warsha hiyo inakuwa chachu ya kufanikisha shughuli za utekelezaji wa mradi sambamba na juhudi za kitaifa na kimataifa za kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.

“Ninafahamu kwamba warsha hii imewakutanisha pamoja wataalam kutoka wizara za kisekta, taasisi za serikali, mamlaka za serikali za mitaa, washiriki wa maendeleo, asasi zisizo za kiserikali na sekta binafsi. Nyinyi ni miongoni mwa wataalam wachache ambao tunatarajia kuwa mabalozi wa kufuatilia shabaha za kupambana na uharibifu wa ardhi katika sekta zenu, huku mkiangalia mbinu za usimamizi shirikishi za kuondoa uharibifu wa ardhi.

Ni dhahiri kuwa tusipofanya kazi kwa ushirikiano kama ambavyo tumeitwa hapa, tutashindwa kufanikiwa. Hivyo, niwaite nyie kuwa 'you’re the champions of LDN na ILAM,' mabalozi wa utekelezaji wa shabaha za kupambana na uharibifu wa ardhi na hivyo kunusuru nchi yetu na ukame na jangwa,” alisema Dkt. Paulo.

Awali, Mratibu wa Mradi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – TFS, Zainabu Shabani Bungwa, akisoma hotuba kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, alitoa shukrani kwa Shirika la FAO na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano wao katika kutekeleza mradi huu, ambao unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira ya Dunia (GEF).

“Lengo kuu la mradi ni kukomesha na kubadili mwelekeo mbaya wa uharibifu wa ardhi na upotevu wa bioanuwai katika maeneo yaliyoharibiwa ya misitu ya miombo kusini-magharibi mwa Tanzania. Utatekelezwa katika maeneo ya Tabora (Kaliua Landscape) katika Wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge; Katavi (Mlele Landscape) kwa thamani ya dola za Marekani milioni 6.875, sawa na shilingi bilioni 16.8, kwa kipindi cha miaka mitano (2022-2027),” alisema Kamishna Msaidizi huyo.

Aliongeza kuwa moja ya shughuli za mradi huo ni kujenga uwezo wa wataalam na sekta mbalimbali katika masuala ya usimamizi shirikishi ili kuhakikisha huduma za kiokolojia kutoka katika Misitu ya Miombo zainaimarika. Alisisitiza kuwa mradi huu tutapiwa kwa uzalishaji bora wa asali na mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki na mengine ya kilimo.

Aidha, watalam watawezeshwa pia tathmini ya rasilimali za misitu, na manunuzi ya baadhi ya vitendea kazi katika maeneo yao. Huku akizitaja shughuli nyingine kuwa ni urejeshwaji wa ardhi iliyoathiriwa, mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi, ujenzi wa vituo vya ulinzi wa misitu (ranger posts), Vituo vya kukusanya na kuchakata asali, nyumba za kufugia nyuki (bee cages) na kuwezesha upatikanaji wa vyanzo vya maji na vituo vya utunzaji wa mbegu za miti na kilimo.

Kwa kumalizia, Kamishna Msaidizi Bungwa aliwashukuru wote waliowezesha kikao hicho na kuhimiza kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha uhifadhi wa misitu, ufugaji wa nyuki, na utalii.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wajumbe wapatao 40.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.