Habari za Punde

Kilele cha Tamasha la Vitabu na Siku ya Kisomo Duniani lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua madhubuti na zaharaka kwa  kuweka mazingira bora ya huduma za Maktaba ili kuwarahisishia wanafunzi kuweza kujifunza mambo mbali mbali pamoja na kutoa elimu iliyobora kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Kilele cha Tamasha la Vitabu na Siku ya Kisomo Duniani lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Amesema kuwepo kwa Tamasha la Vitabu kutasaidia kuenzi utamaduni wa kusoma, kuandika na kuhamasisha jamii kupenda kusoma vitabu mbali mbali kama nijia moja wapo muhimu inayosaidia kufungua milango ya maarifa, ufahamu, ujasiri na kupata ustawi mzuri wa maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa Maktaba kubwa na ya kisasa katika eneo la Maisara ambayo itatoa huduma kwa njia ya kidijitali itakayorahisisha huduma ya upatikanaji wa vitabu na kutanua wigo mpana wa usomaji wa vitabu kwa wananchi sambamba na kujenga Maktaba nyengine sita ( 6 ) kwa Unguja na Pemba.

Aidha ameitaka Bodi ya huduma za Maktaba Zanzibari kusogeza huduma zao kwa wananfunzi wa vyuo vya Mafunzo, Vituo vya kulelea watoto mayatima pamoja na watoto waliolazwa mahospitalini ili waweze kujiendeleza na masomo yao pamoja na kujiongezea maarifa pindi watakapo kuwepo sehemu kama hizo ikiwa ni miongoni mwa haki yao ya msingi.

Saambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa wito kwa watendaji wa Huduma za Maktaba kuendelea kuimarisha zaidi huduma za Maktaba ili wananchi wengi zaidi waweze kupata hamasa ya kuweza kujisomea pamoja na kujiongezea ujuzi wa  aina mbali mbali utakaowasaidia katika maisha yao na jamii kwa ujumla.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema dhamira ya Rais Dkt Hussen Mwinyi ya kuwekeza katika sekta ya elimu ni kuhakikisha anaondoa ujinga Zanzibar na kuiacha ikiwa na wataalamu lukuki wa fani mbali mbali kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mhe. Lela amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa kuruhusu ujenzi wa Maktaba kwa Wilaya  zote za Zanzibar, kupatiwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa sambamba na kuiwezesha Maktaba Kuu kuweza kutumia mfumo wa kidijitali katika kutoa huduma zake na kuweza kumfikia mwananchi popote alipo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar Ndugu Ulfat Abdulaziz Ibrahim amesema madhumuni ya kufanyika kwa Tamasha la Vitabu ni kuihamasisha jamii juu ya matumizi ya huduma za Maktaba, kujenga tabia ya kusoma vitabu mbali mbali ambavyo vinawajengea uwelewa mpana jamii hasa wanafunzi wa skuli.

Mkurugenzi Ulfat amesema Maadhimisho haya yanalenga kuielimisha jamii kuweza kuona umuhimu wa kusoma vitabu na kuwahimiza watoto kujenga tabia ya kwenda Maktaba kujisomea  ili kuwaongezea maarifa na ujuzi kwa ustawi wa maisha yao.

Mapema makamu wa pili wa rais wa zanzibar alikagua mabanda ya maonesho na kujionea shughuli mbali mbali zinzofanywa na wahudumu wa Maktaba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.