SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea kukuza
mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji pamoja na kuweka mkazo wa kurahisisha
michakato, kuimarisha mifumo ya udhibiti na kutoa motisha za kuvutia uwekezaji nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk.
Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipofungua maonesho ya Utalii na Uwekezaji
Zanzibar, 2024 huko viwanja vya maonesho ya Biashara Nyamanzi Wilaya ya
Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa kupongeza
mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya nane anayoiongoza.
Amesema, Zanzibar imefungua milango wazi kwa fursa za biashara
na uwekezaji na tayari imewakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nao kwenye maono
ya ukuaji wa Uchumi endelevu na ustawi wa utalii wa muda mrefu.
Amesema, maonesho hayo yamedhihirisha thamani ya ushirikiano
baina ya wadau wa utalii nchini, Sekta ya Umma na Kibinafsi (PPP) na kueleza kuwa
ushirikiano wao ni njia muhimu za kufikia malengo ya pamoja.
Rais Dk. Mwinyi aliwashauri wadau wa Utalii kuendeleza utamaduni
na shauku ya kufanya Maonesho ya Utalii na Uwekezaji si kwa mnasaba wa Zanzibar
pekee bali kwa Afrika Mashariki na medani za kimataifa ili kuendelea kuitangaza
nchi na vivutio vyake duniani kote.
Alisema, hatua hiyo itaiwezesha Zanzibar kuwa kituo bora cha
ushindani kwa utalii kwenye ramani ya dunia.
Pia, Dk. Mwinyi amesema maonesho hayo ni fursa nzuri za
kubadilishana uzoefu, kuweka harambee, misingi ya miradi ya kuleta mabadiliko
kwenye sekta ya utalii nchini na kuwahimiza wadau wa utalii kushiriki
kikamilifu na kuchangia katika kuunda mustakabali wa utalii na uwekezaji
Zanzibar.
Ameeleza kuwa maonyesho hayo yanaashiria mwanzo wa mashirikiano
mapya na wa kudumu na ubunifu tu sio dhamira ya utalii na uwekezaji peke bali
ari ya pamoja ya kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa kinara wa ukuaji endelevu,
uhifadhi wa utamaduni na maendeleo ya kiuchumi.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi amesema Sekta ya utalii
licha ya kuwa ni utii wa mgongo wa pato la Uchumi wa nchi lakini, inaakisi
nadharia nzima ya maisha ya Wazanzibari, elimu kwa vizazi vilivyopo pamoja na
kuhifadhi utamaduni wa utambulisho wa taifa.
Dk. Mwinyi alibainisha kwamba faida za utalii na uwekezaji zinufaishe
visiwa vyote vya Unguja na Pemba kwa kutengeneza fursa kwa watu wote.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Waziri wa Utalii na Mambo ya
Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amepongeza juhudi za Maendeleo zinazofanywa na
Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopo kwenye sekta ya
Utalii ni kazi kubwa inayofanywa Dk. Mwinyi.
Aidha, amelielezea miaka minne ya mafaniko kwenye uongozi wa Dk.
Mwinyi imeakisi maendeleo enedelevu ya Sekta ya utalii na kukuza biashara na uwekezaji
nchini.
Maonesho hayo ya Utalii na uwekezaji Zanzibar, 2024 yameandaliwa
kwa ushirikiano na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kamisheni ya Utalii, na
sekta binafsi.
Katika hafla hiyo pia kulisainiwa makubaliano ya Ushirikiano baina
ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji na vitega Uchumi, ZIPA katika
kuendeleza kazi za utalii na kurahisisha uwekezaji kwa kuendeleza vivutio vipya
kwa maeneo ya utalii nchini na makubaliano baina ya Kamisheni ya Utalii
Zanzibar na Baraza la Sanaa Zanzibar katika kuondosha changamoto zinazotokana
na utalii, hususan eneo muziki, sana ana burudani.
IDARA
YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment