Habari za Punde

Maafisa Vifungo Vya Nje Wapewa Laptop

Na Mwandishi Wetu, Singida

Jumla ya Maafisa Probesheni Ishirini na Sita wamekabidhiwa kompyuta kila mmoja ili kuendana na kasi ya Uendeshaji wa Mashtaka kwa kutumia mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  ambapo sasa mfumo mpya wa teknolojia unaojulikana kama E-Case Management System ndio unaotumika nchini ikiwa ni lengo la kuharakisha mwenendo wa mashtaka mbalimbali.

Kompyuta hizo zimekabidhiwa mkoani Singida  na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Kazi za Idara ya Huduma za Uangalizi ulioshirikisha Maafisa Probesheni wa mikoa ishirini na sita nchini huku wakisisitizwa kuhifadhi na kutunza vifaa hivyo sambamba na kulinda taarifa za siri zitakazokuwepo katika vifaa hivyo.

‘Naomba mvitunze vifaa mlivyopewa itakua si vizuri baada ya muda mfupi tusikie vifaa hivyo vimearibika au vimepotea lakini kumbukeni pia thamani ya hivyo  vifaa inaenda sambamba na  taarifa muhimu za serikali zitakazohifadhiwa humo  kwahiyo nawaomba pia mvitunze ili kuepuka kuvuja kwa taarifa hizo ambazo ni nyeti sana.Niwakumbushe tu haya tunayotekeleza ni maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo ameagiza mifumo ya vyombo vyote vya haki jinai kusomana ili kuharakisha mienendo ya kesi mbalimbali.’ amesema Dkt. Maduhu

Akizungumza wakati wa mkutano huo uliotanguliwa na semina mbalimnbali za mafunzo kwa maafisa hao wanaoshughulika na vifungo vya nje, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Uangalizi, Charles Nsanze amesema wamenunua kompyuta hizo ambazo zitasaidia utendaji kazi wa maafisa hao ambayo ukosefu wa kompyuta ilikua ni changamoto kubwa hasa ukizingatia idara hii ni moja ya taasisi ambayo iko kwenye mnyororo wa haki jinai lakini pia wizara iko kwenye hatua ya kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa wafungwa ili mfumo huo usaidie kusomana na taasisi zingine za haki jinai.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.