Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali mbalimbali
ya wabunge bungeni jijini Dodoma leo tarehe 12 Juni 2025.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Mradi wa kufua Umeme wa Bwawa wa Julius Nyerere uliopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2115 unatarajiwa kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema hayo wakati
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Donge Mhe. Soud Mohammed Jumah aliyetaka
kufahamu ni kwa kiasi gani mradi huo umechangia matumizi ya nishati safi ya
kupikia na kuepuka ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Akiendelea
kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis amesema tayari Serikali imesambaza huduma
ya umeme wa uhakika mijini na vijijini hatua itakachagiza matumizi ya nishati
safi ya umeme na kuacha kutumia kuni na mkaa.
Alisema Serikali imeendelea kutoa elimu
ya mazingira, kusimamia utekelezaji wa Muongozo wa Taifa wa Matumizi endelevu
ya Ardhi Eneo la Hifadhi ya Mita Sitini kutoka kwenye vyanzo vya maji pamoja na
kuunda Kamati za Mazingira kwa ajili ya kudhibiti uharibifu wa mazingira kwenye
vyanzo vya maji.
Alisema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mhe. Soud
aliyeuliza kuna mkakati gani wa kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mradi wa
Bwawa la Nyerere ili kuhakikisha uendelevu wa mradi.
“Ushirikishwa wa wananchi waishio karibu na mradi huo unafanyika wa kiasi kikubwa na tumewapa jukumu la kutunza mradi na pia tunawahimiza kupanda miti ambayo haikaushi maji, vilevile tunashirikiana na maafisa wa mazingira na mabalozi wa mazingira, lakini pia tunawahamisha mara kwa mara wafanye usafi ili eneo la bwawa liendelee kuwa safi,“ alisema.
Kwa upande
mwingine, alisema Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wanaojihusisha na
vitendo vya ukataji miti hususan maeneo yanayozunguka miradi mikubwa na vivutio
vya utalii hususan Mlima Kilimanjaro.
Alitoa kauli
hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi
kuhusu hatua gani Serikali inawachukulia hatua wanaokata miti katika hifadhi ya
Mlima Kilimanjaro.
Itakumbukwa
kuwa Mradi wa Bwawa la Nyerere unalenga kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) kuwa asilimia 80 ya Watanzania
kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Hivyo, hizo ni juhudi za Serikali chini ya Rais Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amewa kinara katika kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
No comments:
Post a Comment