Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Shaibu Hassan Kaduara, amezindua rasmi awamu ya pili ya Maonyesho ya Madini (Lindi Mining Expo) mkoani Lindi, yakilenga kuvutia wawekezaji na kutangaza fursa mbalimbali za rasilimali madini zinazopatikana mkoani humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Kaduara alisema thamani ya dhahabu imeendelea kupanda katika soko la dunia kutokana na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine, ambako dhahabu inayozalishwa na Urusi imewekewa vikwazo kuingia katika masoko ya kimataifa.
"Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya 1996, pamoja na Sera ya Maendeleo ya Viwanda ya 1996–2020 na ile ya Viwanda Vidogo ya mwaka 2003, zipo kwenye mchakato wa kupitia upya kwa lengo la kuendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo ya kimkakati," alisema Kaduara.
Waziri huyo alibainisha kuwa miradi ya madini ni miongoni mwa miradi ya kimkakati nchini, ambayo inaendelea kufanyiwa tathmini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sera mpya itakayowezesha Watanzania kunufaika zaidi na sekta hiyo.
Lindi Yajitokeza Kama Kitovu cha Madini Nchini
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainab Telack, alisema mkoa huo umebarikiwa kuwa na rasilimali kubwa za madini ambazo tayari zimeanza kuwanufaisha wananchi moja kwa moja.
“Maonyesho haya yanafungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Yanachochea uchumi wa eneo hili na kuongeza thamani ya madini tunayochimba,” alisema RC Telack.
Aliongeza kuwa maonyesho ya awamu ya kwanza mwaka 2023 yalivutia wageni kutoka mataifa 14 na zaidi ya watu 6,000 walihudhuria, jambo lililoongeza hadhi ya Lindi kama eneo la kimkakati kwa shughuli za madini nchini.
“Kwa sasa tunaona ongezeko la wawekezaji, uboreshaji wa miundombinu na fursa za ajira, hali inayodhihirisha kuwa Lindi ni sehemu muhimu katika ajenda ya maendeleo ya taifa,” aliongeza.
Ongezeko la Wachimbaji na Teknolojia ya Uchimbaji
Kwa mujibu wa Mratibu wa Maonyesho hayo, Bw. Mwinjuma Mkungu, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi mkoani Lindi, idadi ya wachimbaji imeongezeka kutoka 2,265 hadi 2,948 baada ya maonyesho ya kwanza, huku mitambo ya kisasa ya uchimbaji ikiongezeka pia.
“Tumeona ongezeko kubwa la wawekezaji na mapato ya serikali yameongezeka kwa asilimia 10.1 baada ya maonyesho ya awali. Hii inaonyesha mchango wa moja kwa moja wa maonyesho haya kwa uchumi wa taifa,” alisema Mkungu.
Alfred Chilumba, mchimbaji mdogo, alishuhudia mabadiliko makubwa baada ya kupata elimu kupitia maonyesho ya awali.
“Tulikuwa hatujui kama tunaweza kutumia mitambo ya kisasa. Maonyesho haya yametufungua macho,” alisema.
Anna Milanzi, mama lishe anayehudumu kwenye maonyesho hayo, alisema ametumia fursa ya ongezeko la wageni kuongeza kipato chake.
“Kwa siku za kawaida napika kilo 5 za unga, lakini leo nimepika kilo 15. Biashara imenoga,” alisema kwa furaha. Maonyesho Yadumu kwa Siku Kadhaa
Maonyesho hayo ya siku kadhaa yanahusisha maonesho ya bidhaa za madini, teknolojia mpya za uchimbaji, warsha za kitaalamu, na majadiliano baina ya serikali, wawekezaji na wachimbaji wadogo.
Yamebeba kauli mbiu: “Madini na Uwekezaji wa Fursa za Kiuchumi Lindi – Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025”, yakisisitiza uhusiano kati ya maendeleo ya sekta ya madini na ushiriki wa wananchi katika mustakabali wa taifa.
No comments:
Post a Comment