Na.Khadija Khamis, WHVUM.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Ndugu Fatma Hamad Rajab amevitaka vyombo vya Habari kufanyakazi kwa kuzingatia maadili hasa katika kipindi hicho cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Aliyasema hayo wakati akikagua mitambo mipya ya kurikodi maudhui pamoja na ufuatiliaji wa taarifa za matangazo ya Radio,Televisheni na Mitandao ya kijamii huko Katika Ofisi za Tume ya Utangazaji Zanzibar, Kilimani, Wilaya ya Mjini .
Alisema kuwa ni vyema vyombo vya habari kuzingatia miongozo na kanuni za Tume ya Utangazaji ili kuepusha vichocheo vya uvunjifu wa Amani nchini .
Aidha aliwataka wafanyakazi wa Tume hiyo kuacha muhali wakati wa utekelezaji wa kazi zao ili kusiwe na upendeleo wala kudhulumiwa mtu katika utekelezaji wa sheria.
Nae Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Hijji Dadi Shajak alilishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa msaada mkubwa wa mitambo hiyo jambo ambalo limerahisisha ufanisi wa kazi .
Alifahamisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Tume ya Utangazaji, Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Uhalifu wa Mtandao (Cyber Crime) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na TEHAMA Khamis Ali Haji alisema mitambo hiyo inarikodi taarifa zote zinazotolewa na vyombo vya habari vya Zanzibar pamoja na mitandao yote ya kijamii ili kuchukua hatua stahiki kwa chombo chochote kinachokwenda kinyume na kanuni na sheria za Tume ya Utangazaji Zanzibar.
Amesema mitambo hiyo itarahisisha kupokea ujumbe kwa wakati na kusaidia kuchukuwa hatua za haraka pindi kukijitokeza ukiukwaji wa kanuni na sheria za Tume ya Utangazaji katika vyombo vya habari .
No comments:
Post a Comment