Habari za Punde

WAZIRI MKUU AKAGUA MIUNDOMBINU YA MABASI YAENDAYO HARAKA JIJINI DAR ES SALAAM


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza wakati alipokagua Miundombinu ya mabasi yaendayo haraka  katika kituo cha Kivukoni jijini Dar es salaam, Oktoba 2, 2025. Wengine kutoka kushoto ni Naibu Waziri  Ofisi ya Rais TAMISEMI, Zainabu Katimba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albart Chalamila , Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa  na  Mkurugenzi Mkuu wa MOFAT, Abdallah Kassim.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mashine za malipo za kielektroniki alipokagua Miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika Kituo cha Kivukoni jijini Dar es salaam, Oktoba 2, 2025.  Kulia kwake ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa na kushoto kwake ni Mkuu wa moka wa Dar es salaam, Albart Chalamila.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua moja  ya mabasi 60 ya   kampuni ya MOFAT  yaliyoanza kutoa usafiri  kwa abiria wa mwendokasi katika njia  ya Kivukoni Kimara, Gerezani na Morocco jijini Dar es salaam, Oktoba 2, 2025. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MOFAT,  Abdallah Kassim.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza kikao cha Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais  TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na viongozi wa  TRA, DART, UDART,  TPDC na Msemaji Mkuu wa Serikali cha kujadili mwenendo na maboresho ya huduma za mabasi yaendayo haraka. Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es salaam, Oktoba 2, 2025.


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua kuingiza mabasi 60 mapya kwenye Barabara ya mabasi yaendayo haraka njia ya Kimara hadi Kivukoni iliyokuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi ili kukabiliana na upungufu wa magari uliokuwepo.

 

Amesema kuwa idadi hiyo itafanya njia hiyo kuwa na mabasi 90 ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuondoa kero ya usafiri iliyokuwepo katika kipindi cha hivi karibuni.

 

Amesema hayo leo Alhamisi ( Oktoba 02, 2025) alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri kwa mabasi yaendayo haraka kwa njia ya Kivukoni hadi Kimara jijini Dar es Salaam.

 

"Serikali yenu baada ya kuruhusu makampuni binafsi tumeona tuchukue mabasi 60 kutoka kampuni ya Mofat yaingie katika barabara hii na yameanza kutoa huduma leo, malengo yetu ni kuondoa kadhia ya usafiri kwenye njia hii"

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza UDART na DART kuhakikisha wanasimamia matumizi ya kadi za kielektroniki katika utozaji wa nauli badala ya kutumia fedha taslimu (Cash) ili kudhibiti upotevu wa mapato katika usafiri huo.

 

"Na tumeagiza kadi hizi zisiwe za mabasi haya pekeyake, tunataka zitumike kwenye viwanja vya mipira, usafiri wa Azam marine, SGR, vituo vya mabasi, Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Jerry Silaa, tunataka hili likamilike kwa haraka"

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Taasisi ya Dart  kuhakikisha wanasimamia kikamilifu usafiri huo ili kupunguza kero ya usafiri wa mabasi hayo katika jiji la Dar es Salaam.

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuiamini Serikali kwamba itahakikisha kero ya usafiri katika njia hizo itapunguzwa kwa kiasi kikubwa ili kuondoa tatizo la usafiri katika jiji la Dar es Salaam. "Haya yaliyojitokeza tuamini sasa yamekwisha"

 

Akizungumzia kuhusu maboresho hayo, Mmoja ya wasafiri amesema kuwa usafiri katika siku hiyo umekuwa wa kuridhisha na wanasafiri kwa wakati “Kwasiku ya leo usafiri umekuwa mzuri na magari yameingia kwa wakati”

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                     

JUMANNE OKTOBA 02, 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.