Habari za Punde

Walimu ni Nguzo ya Maendeleo - MAJALIWA *Asema Walimu ni fahali ya nchi na chimbuko la uvumbuzi na ubunifu *Dkt. Biteko asema ualimu ndio taaluma inayomtengeneza mtu awe bora kuliko hata ualimu wenyewe

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakimsikiliza Mkurugenzi wa Makampuni ya Jembe, Sebastian Ndege walipotembelea mabanda ya maonesho ya makampuni hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari  Ushirombo wilayani Bukombe

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa walimu ni nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote hapa duniani kwani ndio wanaotoa rasilimaliwatu yenye elimu ambayo ni muhimu zaidi ya Taifa.

Amesema kuwa mafanikio ya kielimu, kijamii na kiuchumi yanatokana na juhudi za walimu kwani walimu ni fahari ya familia, jamii na nchi na kupitia mikono yao vijana wa kitanzania wanajengewa maarifa, stadi na maadili ya uzalendo.


Amesema hayo leo Ijumaa (Oktoba 03, 2025) wakati wa maadhimisho ya siku mwalimu duniani ambayo kiwilaya imeadhimishwa Bukombe mkoani Geita katika uwanja wa shule ya sekondari ya ushirombo.


"Kila hatua ya ustawi wa kijamii na kiuchumi inaanzia darasani kupitia juhudi na maarifa ya walimu. bila walimu, hakuna taaluma, hakuna viongozi wa kesho na hakuna Taifa linaloweza kusimama imara, walimu ndio chimbuko la uvumbuzi na ubunifu wa kizazi kipya.".


Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kada ya ualimu hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kada hiyo ikiwemo kwa kupandisha madaraja na kuimarisha mafunzo kwa walimu.


Ameongeza kuwa ili kukabiliana na upungufu wa walimu nchini Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuthamini na kuwekeza katika kada ya ualimu kwa kuajiri walimu wapya kila mwaka. 


"Taarifa za Mkoa wa Geita zinaonesha wazi kuwa idadi ya walimu imeongezeka kutoka 11,646 mwaka 2021 hadi kufikia walimu 13,379 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 14.8".Katika mwaka 2024/2025, zaidi ya walimu 7,500 wa shule za sekondari na msingi wamepandishwa madaraja yao"


Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi ya Rais - UTUMISHI kufanya msawazo wa walimu ndani ya mikoa husika kwa kuhakikisha kila shule inapata walimu ili watoto wa kitanzania wapate elimu bora.


"Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Vyuo vya Ualimu na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imarisheni mafunzo ya kitaaluma na endelevu kwa walimu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya dunia ya leo".


Naye, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa taaluma ya ualimu ndio taaluma pakee inayomtengeneza mtu awe bora kuliko hata ualimu wenyewe na wakati wowote hujinyima muda wake na nguvu zake zote kumtengeneza mtu kuwa mume au mke bora au hata mzazi bora.


"Taaluma ya ualimu humfanya mtu kuwa raia mwema kwenye nchi na zaidi sana humfanya kuwa mtumishi, mfanyakazi na mzalishaji mali bora, wakati wote wa maisha yake, hii ni taaluma ambayo tunaamini ni ya uumbaji wa pili baada ya mwanadamu kuzaliwa na wazazi wake, kazi ya pili huendelea hapa duniani na muumbaji huwa ni mwalimu"


Ameongeza kuwa Mwalimu ndiye anayetoa mwelekeo wa maisha ya kila mtu na ukiona jamii yoyote yenye ustaarabu na kustaarabika huhitaji kupiga ramli kujua nani chanzo chake bali mwalimu ndio sababu yake


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline Nombo amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kufanya shughuli mbalimbali zinazowawezesha walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya ikiwemo ujenzi wa miundombinu shuleni na lengo ni kukuza ujifunzaji na ufundishaji.


Amesema kuwa Serikali inathamini jitihada zunazofanywa na walimu kwani wamekuwa kiini cha mafanikio. "Kila mmoja wetu amepita kwenye mikono ya walimu, tunawashukuru walimu wote wanaotoa nguvu na maarifa yao kuwawezesha watanzania"

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipowasili kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo  wilayani Bukombe ambapo alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani, Oktoba 3, 2025. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakiingia kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari  Ushirombo wilayani Bukombe ambapo Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani, Oktoba 3, 2025. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Marten Shigella.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo wilayni Bukombe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani kwenye uwanja wa  Shule ya Sekondari Ushirombo  wilayani Bukombe.
Walimu wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo wilayani Bukombe, Oktoba 3, 2025. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Marten Shigella. 
Washiriki wa Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani wakiwasha tochi za Simu zao kuashiria kuwa elimu ni mwanga katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo wilayani Bukombe, Oktoba 3, 2025. Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Washiriki wa Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani wakiwasha tochi za Simu zao kuashiria kuwa elimu ni mwanga katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo wilayani Bukombe, Oktoba 3, 2025. Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. 
Walimu wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo wilayani Bukombe, Oktoba 3, 2025. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Marten Shigella.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.