Habari za Punde

ABDI KASSIM "BABI" AFUZU MAJARIBIO YA SOKA LA KULIPWA VIETNAM

KIUNGO wa Yanga ya Dar es Salaam,  na Timu za Taifa za Tanzania na Zanzibar, Abdi Kassim ‘Babi’ amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya Dong Long Tam An FC ya Vietnam.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Maulid Hamad Maulid alisema kwa simu jana kutoka Zanzibar kuwa mchezaji huyo amewajulisha kuwa amefuzu majaribio hayo.

Alisema waliwasiliana na Babi juzi kumuulizia kwa vile yupo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ ambacho kitashiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo jijini Dar es Salaam.

“Babi ametujulisha kuwa amefuzu majaribio yake, hivyo kila kitu kimeenda vizuri, tunamtakia kila la heri.

“Atawasili Dar es Salaam Jumatatu na ataungana kambini na wenzake kwa ajili ya mchezo utakaofuata wa Chalenji dhidi ya Rwanda, lakini huu wa kwanza dhidi ya Sudan Jumapili hatauwahi,” alisema Maulid.

Alisema masuala mengine baada ya kufuzu majaribio hayo yatahusiana na mambo ya maslahi kati ya Yanga ya Dar es Salaam anayoichezea Babi kwa sasa.

Tayari mwanzoni mwa wiki hii Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema kuwa kama Babi atafuzu majaribio, klabu yake itamuachia baada ya kupewa kiasi cha Sh milioni 100.

Nchunga alisema watamruhusu endapo watapewa kiasi hicho na kama timu hiyo haitakuwa tayari kutoa fedha hizo suala la usajili wake watalifunga.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.