Na Rajab Mkasaba Tripoli, Libya
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein leo ameungana na viongozi wakuu wa nchi za Afrika, Jumuiya ya Ulaya EU na nyeginezo waalikwa, katika ufunguzi wa Mkutano wa tatu wa mashirikino kati ya Umoja wa Afrika na JumuIya ya Ulaya EU.
Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika mjini Tripoli, Libya, umehudhuriwa na zaidi ya viongozi wakuu 80 wa nchi mbali mbali. Mkutano utazungumzia juu ya mashirikiano yaliopo kati ya Afrika na nchi za Jumuiya ya Ulaya sanjari na suala zima la siasa.
Aidha, katika mkutano huo, suala la amani na usalama pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, maendeleo ya sekta binafsi, miundombinu, umeme, kilimo, sayansi, ICT, usalama wa chakula na uhamiaji pia, yanatarajiwa kuzungumzwa.
Maudhui makuuu ya Mkutano huo ni kuimarisha suala zima la uwekezaji, ukuaji wa uchumi pamoja na ajira.
Katika ufunguzi wa Mkutano huo, Kiongozi wa Libya Mhe. Mu'ammar Gaddafi alieleza kuwa Afrika na Ulaya zina historia kubwa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo. Alieleza kuwa wakati umefika kwa nchi za Ulaya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Afrika katika kuimarisha sekta za maendeleo.
Kiongozi huyo alieleza kuwa juhudi za kushirikiana katika sekta muhimu ya uchumi ni suala muhimu katika maendeleo ya pande zote mbili, hivyo kuna kila sababu ya kuiimarisha sekta hiyo kwa kuweza kukuza mashirikiano yaliopo.
Aidha, alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbali mbali zinazoikabili bara la Afrika, Ulaya na hata dunia kwa jumla ikiwemo changamoto ya kupambana na ugaidi, Kiongozi huyo alieleza kuwa mashirikiao ya pamoja yanahitajika katika kupambana na kadhia hiyo.
No comments:
Post a Comment