Habari za Punde

IT EFFICIENT YAKABIDHI KOMPYUTA 29 KWA SKULI SITA ZANZIBAR.

Na Salum Vuai


KAMPUNI ya IT Efficient yenye makao makuu yake nchini Uingereza kwa kushirikiana na Mjumbe wa chuo cha ufundi cha Karume Zanzibar Simai Mohammed Said, wametoa msaada wa kompyuta 29 kwa skuli sita hapa nchini.

Kompyuta hizo zilikabidhiwa juzi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwanaidi Abdallah Saleh huko afisini kwake Mazizini, na baadae yeye kuzikabidhi kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Haji Abdulhamid kwa niaba ya skuli nyengine.

Skuli zitazofaidika na msaada huo uliogharimu shilingi 8,700,000 ni Karume, Darajani, Haile Selassie, Ben Bella, Hamamni na Vikokotoni.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya IT Efficient Piersen Austin, Simai alisema lengo la kutoa msaada huo ni kusaidia azma ya serikali kuwawezesha wanafuinzi wote wa Zanzibar kupata taaluma ya kompyuta.

Alisema kutokana na umuhimu wa kompyuta katika ulimwengu wa kisasa unaokwenda kisayansi, ni vyema wananchi wengine wenye uwezo wahamasike kutoa mchango wao ili kuunga mkono mikakati ya serikali ambayo lengo lake ni kuwajengea wanafunzi msingi mzuri wa kumudu ushindani wa kisoko wanapohitimu masomo.

Simai alitoa wito kwa Wazanzibari walioko nje kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika nchi yao kwa kutoa misaada kama hiyo, ili kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua ya maendeleo kama zilivyo nchi nyengine.

Aidha alieleza yapo maeneo mengi yanayohitaji kusaidiwa ikiwemo sekta ya afya, na kwamba misaada watakayoitoa ina mchango mkubwa katika kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii.

Akitoa shukurani zake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwanaidi Saleh Abdallah, alisema serikali inathamini michango ya wananchi na wahisani wanaokubali kutoa misaada, ikifahamu kuwa wana nia njema na nchi hii.

Aliwaomba wafadhili hao kutoishia hapo bali kuangalia maeneo mengine wanayoweza kusaidia ili kuzipa nguvu jitihada za serikali katika kuinua ufahamu wa wanafunzi wa visiwa hivi.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Haji Abdulhamid, akishukuru kwa niaba ya skuli zilizonufaika na msaada huo, alisema kompyuta hizo zitaongeza ari ya wanafunzi kutaka kujua kwa undani namna ya kuzitumia hali itakayoinua uwezo wao kimasomo.

Aliahidi kuwa kompyuta hizo zitatumika kwa lengo lililokusudiwa ambapo pia litawashajisha walimu wengine kutanua ufahamu wao.

Chuo cha Mbweni kitapata kompyuta 19, huku skuli za Darajani, Benbella, Haile Selassie, Hamamni na Vikokotoni zikipata kompyuta mbili kila moja.

1 comment:

  1. Mara nyingi panapotokea neema ya misaada ya kimaendeleo, kama huu wa vifaa vya kitecknolojia (computers) wanaokabidhiwa vifaa kama hivyo, husau kuwa Zanzibar ni pamoja na Pemba.

    Niliposoma taarifa hii na kuona hapo awali kabla ya kushuka chini, nilikuwa na mawazo kwamba katika magao wa computer hizo, japo saba zingalikwenda katika kisiwa cha Pemba.

    Kusema kweli ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Pemba ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa cha maendeleo ya Zanzibar, kwa vile ndiyo inayozalisha zao kuu la uchumi wa visiwa hivyo, kwamba inaachwa nyuma kimaendeleo na kunyimwa misaada kama hiyo ambayo imetolewa kwa ajili ya Zanzibar na siyo Unguja.

    Hali hii bado itakuwa haijengi ule umoja tuliuanza baada ya chaguzi kuu na kuundwa kwa serikali ya umoja, kwani itatokea kuwapa imani mbaya watu wa Pemba na wao kuanza kutafuta misaada kwa ajili yao tu na kuwasahau wenzao wa Unguja.

    Mohammed

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.