Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuhakikisha vyombo vya habari vinaimarika ili kurejesha haiba yake iliyokuwa ikitambulikana Kimataifa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ikiwa ni miongoni mwa mikutano yake ya kukutana na wakuu na watendaji wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa Televisheni, Redio pamoja na Gazeti ni vyombo vyenye historia kubwa hapa Zanzibar ambavyo kwa nchi za Afrika Zanzibar ilikuwa ni ya mwanzo kumiliki ikiwa pia ni ya mwanzo kuwa na TV ya rangi kwa nchi za Afrika.
Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo kuna haja ya kurejesha haiba ya vyombo hivyo ili Zanzibar iendelee na uhalisia wake wa kuwa ndio muasisi na muanzilishi wa vyombo hivyo juhudi ambazo zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha sifa hiyo inabaki.
Alieleza kuwa licha ya kuwepo changamoto mbali mbali zinazovikabili vyombo hivyo vya habari lakini juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali ili kuhakikisha vinaimarika zaidi.Aidha, Dk. Shein aliwasisitiza wafanyakazi wa vyombo hivyo nao kubadilika na kuwa wabunifu huku Serikali yao ikifanya juhudi za kuviimarisha vyombo hivyo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza umuhimu wa kutimiza Azimio la Dunia la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2012 vyombo vyote vya habari viwe katika mfumo wa Digitali na kusisitiza kuwa kwa upande wa Zanzibar ipo haja ya mfumo huo kuanza kutekelezwa hivi sasa.
Dk. Shein aligusia haja ya kuwatunza na kuwaenzi wasanii wakongwe sanjari na kuendeleza utamaduni na wasanii wote kwa jumla ili kuweza kuimarisha na kuuendeleza utamadini, wasanii, silka, desturi za Kizanzibari.
Katika mazungumzo hayo pia, Dk. Shein alipongeza juhudi za Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa kazi nzuri waliyoifanya ndani ya miaka mitano na kupongeza kwa kulisimamia na kutengeneza na hatimae kutoa Kamusi la Kiswahi pamoja na vitabu vyengine vya lahaja za Kizanzibari.
Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuwepo mpango mkuu wa masomo kwa wafanyakazi wa sekta za Wizara hiyo pamoja na mpango wa Utafiti kwa lengo la maendeleo ya Zanzibar. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na Idara ya Uchapaji na kueleza kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo katika Idara hiyo.
Akizungumzia juu ya sekta ya Utalii, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea na mikakati yake katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika zaidi ili kuendelea kuchangia uchumi wa Zanzibar.
Nae Makamu wa Rais wa Pili, Balozi Seif Ali Idd alipongeza juhudi zinazochukuliwa na vyombo vya habari pamoja na sekta nyenginezo ziliozomo katika Wizara hiyo na kueleza kuwa licha ya changamoto zilizopo lakini bado zimekuwa zikifanya kazi vizuri.
Balozi Iddi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha Wizara hiyo pamoja na Idara zake vikiwemo vyombo vya habari vinaimarika zaidi.
Nao viongozi wakuu na watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo walipongeza juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ikiwa ni pamoja na mfumo aliounzisha wa kuzungumza na viongozi na watendaji wa Mawizara.
Viongozi hao pamoja na watendaji wa Wizara hiyo walieleza mafanikio, mipango, malengo, miradi, shughuli zilizotekelezwa na zinazotekelezwa, majukumu ya Wizara pamoja na changamoto zinazowakabili.
Wakati huo huo viongozi hao na watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo walimkabidhi, Dk. Shein Kamusi la Kiswahili pamoja na vitabu vya lahaja.
Dk. Shein anatarajiwa kuhudhuria maadhimisho ya mika 49 ya Uhuru wa Tanzania (Bara) zitakazofanyika katika uwanja wa Uhuru mjini Dar-es-Salaam hapo kesho.Katika Sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu atakuwa mgeni rasmi ambapo Gwaride litatoa salamu ya Rais na Mizinga 21 itapigwa.
Aidha, Mhe. Rais na Amiri Jeshi Mkuu atakagua Gwaride na pia, Gwaride kupita mbele yake kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka na hatimae Gwaride litasonga mbele hatua 15 na kutoa salamu ya Heshima na Salamu ya Utii.
No comments:
Post a Comment