WANANCHI wa Shehia ya Sebleni wilaya ya Mjini wamepinga ujenzi wa kituo cha polisi kinachojengwa katika viwanja vya Kibandamaiti kwa kile walichoeleza kuwa eneo hilo ni la wazi na halistahiki kujengwa kituo.
Mmoja ya wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Abdalla Juma Mohammed alisema ujenzi wa kituo hicho cha polisi, katika eneo hilo unaweza kuleta matatizo makubwa kutokana na kuwa eneo hilo, ni la wazi ambalo linastahiki kubaki kama lilivyo kwa ajili shughuli nyingine.
Alisema mbali na kuwa ni eneo la wazi lakini pia hutumika kwa ajili ya michezo pamoja na kuwa ni viwanja maalum kwa ajili ya mikutano ya vyama vya siasa hivyo ujenzi huo unaweza kuzorotesha shughuli hizo kwa kiasi kikubwa.
“Hili eneo tangu zamani lilikuwa linatumika kwa michezo lakini leo limevamiwa na kujengwa, sasa ni wapi wananchi wanaweza kupata viwanja vya kuchezea mpira kwani na wao wana haki’’,alisema.
“Palianza kujengwa skuli ya Sebleni na baadaye skuli ya Muungano na wao wananachi wakawa kimpya, baadaye tukajengewa tangi la maji katikati ya uwanja tukanyamaza, leo tena ujenzi wa kituo cha Polisi sasa tunahoji je! hii michezo tukacheze wapi’’, alihoji
Alisema mbali na mambo hayoo eneo hilo limegeuzwa kituo kikubwa cha kulaza magari wakati wa mcha na usiku jambo ambalo liwanyima haki wananchi wa eneo hilo kutia viwanja hivyo kama ilivyokuwa hapo awali.
Aliongeza kuwa wao hawapingi kujengwa kwa kituo cha Polisi katika eneo lao kwani pia kina faida kubwa kwa vile kitaweza kupunguza uhalifu, lakini ni vyema likatafutwa eneo jingine na hilo kubakia kama lilivyo.
Akizungumzia ujenzi huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Aziz Juma Mohammed, alikiri askari wake kutumika kujenga kituo hicho lakini ni kwa asilimia ndogo ambapo alisema ni kwa kutoa msaada tu.
Alisema kuwa sio kweli kama wao wametumika kujenga kituo hicho lakini ni wananchi wenyewe ndio wanaojenga na askari wake hushiriki kwa asilimia ndogo.
Aliongeza kuwa kama kuna mwananchi yoyote ambaye ana wasiwasi na ujenzi huo basi vyema akapeleka malalamiko yake, ofisi za chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi ambao kwa asilimia kubwa wanahusika na ujenzi huo.
Pia Kamanda Aziz alielezea kusikitishwa na wananchi hao ambao wanapinga kujengwa kwa kituo hicho, na kusema kuwa ni wale miongoni mwa wasiopenda maendeleo
No comments:
Post a Comment