Inahitaji mikakati makini, utekelezaji kwa vitendoMARA baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Saba, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, aliibuka na mikakati anuai ya kuharakisha maendeleo Zanzibar, mojawapo likiwa ni ‘Diaspora’. Pengine dhana hiyo ni mpya katika masikio ya Wazanzibari wa kawaida, lakini wananchi wa Unguja na Pemba, waligundua kwamba Dk.Shein hakuwa akipiga hotuba alipokuwa akiitangaza Diaspora kuwa moja ya mikakati yake, pale alipoiundia ofisi maalum iliyo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu na kuteua Naibu Katibu Mkuu wa kushughulikia hilo tu.
Akiwa kama Rais, Dk.Shein atakuwa amekamilisha jukumu lake na kilichobakia ni kwa watendaji waliopewa kazi kuitekeleza kwa kuelewa kuwa nchi yao akiwemo kiongozi mkuu ana matumaini ya mavuno kupitia diaspora.
Katika waraka huu wa CHOWEA leo, nipendekeze kidogo njia mbali mbali ambazo Zanzibar inaweza kuzitumia kuweza kufanikiwa kupitia diaspora.
Kwa kifupi, napenda tuelewe kuwa diaspora ni kundi la watu ambao wana asili ya sehemu Fulani, lakini wanaishi nje ya nchi yao kwa namna moja ama nyengine, kwa hivyo kwa Zanzibar ‘Diaspora watakuwa ni watu wote wenye asili ya Zanzibar kwa njia moja ama nyengine, ambao wanaishi nje kwa kazi, kuhama, kuoa, kuolewa na hata ukimbizi, bila kujali wana uraia wan chi gani’.
Zanzibar ikiwa ni kisiwa chenye historia ya muda mrefu na nchi iliyopita katika majaribu mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, pamoja na udogo wake, tabaan ina diaspora wengi duniani, ikilinganishwa na nchi za Afrika.
Kuna njia nyingi ambazo Zanzibar inaweza kuzitumia kuweza kuvuna kupitia diaspora, ikiwemo mikutano ya kimataifa kwa diaspora, mialiko ya matembezi, maombi ya huduma za jamii kama afya, elimu na michezo, fedha, pamoja na utaalamu.
Katika kuangalia diaspora wa Zanzibar, tunaweza kukuta kuna makundi tafauti, yakiwemo ya wastaafu walioko majuu, vijana wanaohangaika kimaisha, wasomi wanaofanya kazi za kitaalamu kama wahadhiri wa vyuo vikuu, wahandisi na madaktari.
Kutokana na ma-diaspora wa Zanzibar kuwa na hamu ya kusaidia maendeleo ya nchi yao, kwa vile wengi wao wana jamaa zao wanaoishi Unguja na Pemba, si kazi ngumu hata kidogo kuandaa utaratibu wa kuwaleta nyumbani na kuwaonesha namna wanavyoweza kusaidia maendeleo ya nchi zao na jamaa zao.
Kuna haja ya kuitishwa mkutano mkubwa wa ‘Zanzibar Diaspora’ hapa Zanzibar, ambao utawaalika wazanzibari wote walioko nje kuhudhuria, ambapo naamini kwa maandalizi mazuri na Zanzibar yenye amani ya sasa inayotabulika ulimwenguni kote watakuja.
Hapa hatuna haja ya kufikiria gharama, kwani diaspora hawa watatumia gharama zao wenyewe kwa jinsi wanavyoihamu nchi yao, cha kufanyika ni kupangiwa ukumbi ambapo hata wa hoteli ya Bwawani utawatosha
Ofisi inayohusika na diaspora ni lazima ihakikishe inajikurupusha na kuwa na viunganishi ‘connection’ na Jumuiya zote za wazanzibari ambazo zimeenea ulimwenguni kote na zinajulikana wazi, ili waweze kushirikiana nazo kuandaa kongamano hilo.
Ni imani yangu kwamba, Rais Shein atakubali kulibariki kongamano na hata kulihutubia japo kwa siku ya kwanza kwa vile nae ni muumini wa diaspora kwa maendeleo na amewahi kuwa m-diaspora wa Zanzibar kwa muda mrefu sana.
Bila shaka sina haja ya kukokotoa nini ma-diaspora wetu hawa waambiwe na tuwasikilize wanasemaje, kwani wataalamu wa hayo tunao wengi tu na hawa ndugu zetu nao ni wataalamu tosha wa vipi diaspora inaweza kupeleka maendeleo nyumbani.
Faida ya diaspora imedhirika katika mataifa mengi yaliyokuwa masikini, ikiwemo China, India, Pakistan na nchi nyengine za Asia na Ulaya Mashariki ambazo hivi sasa ziko juu kiuchumi.
Wageni hawa ambao wengine watakuja na familia zao, watapofika nchini watatembelea maeneo mbali mbali na kununua bidhaa tele za hapa nyumbani, ambapo wananchi wetu watapata soko na kujiinua japo kidogo kifedha.
Tutapowaweka na wataalamu wa fani zenye kulingana waliopo nyumbani, ndugu zetu hawa watasikia maeneo tunayotaka kusaidiwa na tabaan watatusaidia japokuwa kwa kuanzia misaada midogo midogo, pamoja na hata kutupa ushauru wa wapi tunaweza kupata misaa, jambo ambalo halitokuwa dogo kwetu.
Kama hatuelewi kuna wazanzibari ambao wamekusanya vitabu vya skuli na kompyuta, wanasubiri waambiwe tu wazilete Zanzibar kugaiwa bure maskuli na ushahidi wa haya wanao viongozi wetu, tena wakubwa tu wanaokwenda ziara za nje, cha ajabu sijui kwa nini hawatoi umuhimu kwa hili.
Kuna madaktari ambao wanathaminiwa na nchi tajiri, kiasi ambacho wanaweza kupewa vifaa vya kusaidia hospitali japo chache za mijini na vijijini, sasa kwa nini tusitumie fursa hii.
Nchi kubwa kubwa ikiwemo Canada, zinatumia wataalamu wa Tekonolojia ya habari (ICT) kutoka Zanzibar ambao ni wenyeji wa kisiwani Pemba, hivyo hawa basi hatuwezi kuwakaribisha nyumbani kusaidia japo mawazo ya vipi nasi tunaweza kuendesha sera za ICT, ambayo hadi sasa ipo ipo tu.
Ofisi inayoshughulikia diaspora inapaswa kufahamu kwamba kuna wazanzibari ambao weshachoka kuishi nje ya nchi yao na hawana shida ya pesa, bali wanataka kuhisi kama wanatakiwa na kuthaminiwa kwao, tukiwaita watakuja na kufanya kazi nyumbani kwao, hiyo nayo ni faida moja ya diaspora.
Mifano hiyo imedhihirika kwa diaspora mbali mbali akiwemo Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, ambae hivi sasa ni waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na madaktari wengine wengi ambao tunawajua, hiyo ndiyo diaspora yenyewe jamani.
Tuache kutawaliwa na fikra za kimasikini na kudhani kila mtu anataka mshahara mkubwa, kwa vile tumekulia katika kulipwa mishahara midogo, diaspora wetu weshapita huko, wao zaidi sasa ni uzalendo.
Kwa wale vijana wetu wa Unguja na Pemba waliosambaa katika kila kona ya ulimwengu ni lazima kuwekwe utaratibu rasmi wa kuwatambua kupitia ofisi zetu za ubalozi, badala ya kuwaacha na kutowatambua kutokana na wao kubadilisha uraia.
Walioishi ‘majuu’ watakubaliana nami kwamba vijana hawa wamefanya hivyo ili kurahisisha njia za kuishi na wamefanikiwa, lakini ukweli wanaipenda nchi yao, hivi sasa inasikitisha tumewaacha na kuwafanya waichukie nchi yao kwa vile kila wanapokwenda kwenye ofisi za kibalozi zetu hufukuzwa kama wageni, lazima diaspora Zanzibar ibadilike katika hili.
Huku ikijitayarisha na kuweka ‘Zanzibar desk officers’ katika ofisi zote za balozi za Tanzania nje, kuna haja kwa sasa kufanya utaratibu wa kuwasiliana nao kupitia ‘conection’ mbali mbali na kuwaelimisha mabadiliko yaliyopo Zanzibar na vipi wanatakiwa kushiriki kusaidia maendeleo.
Njia nyengine ya haraka haraka, ambayo ingweza kufanyika Zanzibar ni kurasimisha njia ya diaspora wa Zanzibar kuwatumia fedha ndugu na jamaa zao, kwani hivi sasa wamekuwa na woga kutokana na fedha zao kupotea na mikato mikubwa wanayofanyiwa na ofisi zilizoenea kuazia Mji Mkongwe hadi Wete, huku Serikali ikiambulia patupu.
Hili si gumu, kwani tukijikumbusha wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifungua benki kwa ajili hiyo Mjini Dar es salaam, ambako ni rahisi kujifunza.
Suala la Diaspora Zanzibar linahitaji kuendeshwa kwa kasi na umakini mkubwa, si tu kwa sababu wazanzibari wote walioko nje ni Watanzania, bali pia ukizingatia kuwa ndugu zao wa Tanzania Bara nao wanatumia dhana hii na wako makini kwa kuwekeza fedha nyingi.
Katika kutafuta pakuanzia kwa ma-diaspora walioko Marekani na Carebbean, ni kufuatilia makubaliano yaliyopitishwa wakati wa ujio ‘African Diaspora Trails’ miaka miwili iliyopita, ambapo kundi kubwa la eneo hilo lilitembelea Tanzania na kuja Zanzibar.
Wengine tulikuwa tunaona hata aibu hata kuuliza ‘kulikoni?, kimya kimetawala tokea kuondoka ndugu zetu hawa ambao walituelekeza namna ya kuendelea kushirikiana nao tena kupitia taasisi yenye kueleweka duniani, tumepata afueni baada ya kusikia Dk.Shein amerasimisha diaspora.
Matumizi ya ICT, fursa za mawasiliano ya anga na ya bahari, yanaweza kusaidia sana katika kuiwezesha Zanzibar kufaidika na diaspora.
Katika kusimamia hili ni lazima watendaji waliopewa majukumu wabadilike na walitizame zaidi katika sekta ya uchumi na kamwe wasitawaliwe na siasa mgando.
No comments:
Post a Comment