SIKU YA UHURU WA HABARI DUNIANI
Na Abdulla Mohammed Juma
KESHO dunia inaadhimisha siku maalum ya uhuru wa vyombo vya habari ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 3 Mei ya kila mwaka, ambapo wanahabari hujikusanya na kufanya tathmini ya masuala mbali mbali yenye kuhusu tasnia hiyo.
Miongoni mwa mambo yanayotizamwa mara nyingi huwa ni changamoto na mafanikio ya fani ya habari duniani, huku idadi ya wanahabari waliopoteza maisha kazini, kufungwa jela na kuonewa au kunyimwa haki kwa njia moja au nyengine hubainishwa na hata kuna wanaoitumia kwa kuwatunza wanahabari bora wa mwaka.
Nikiungana na wanahabari wa Zanzibar katika maadhimisho hayo, kwanza niwapongeze kwa sherehe hiyo adhimu na pongezi nyengine ni kutokana na mchango wao mkubwa katika kufanikisha mchakato wa kujenga Zanzibar mpya, kuanzia kuripoti harakati za kubadilishwa katiba ya Zanzibar hadi kufikia kufanyika kura ya maoni kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.
Jengine kubwa ambalo nalazimika kulitaja ni kwa wanahabari hawa kuchangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia za siasa za Zanzibar, uliendeshwa bila ugomvi wala ghasia, mapigano na machafuko.
Kutokana na matukio hayo makubwa kuendeshwa kwa amani, utulivu na kwa demokrasia pana, tabaan kwa mwaka unaoadhimishwa vyombo vya habari vya Zanzibar navyo havitakuwa vimekumbwa na changamoto mbaya mbaya za kuuawa waandishi au kufungwa jela.
Kwa mantiki hiyo basi, cha kuangaliwa zaidi wakati wanahabari wa Zanzibar wakiungana na wenzao duniani kuadhimisha siku hiyo ni kujitathmini namna gani wanatoa mchango wao katika kuijenga Zanzibar mpya yenye maendeleo endelevu, amani ya kudumu, kuimarisha umoja na mshikamano.
Kama uchaguzi umekwenda vyema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa imeundwa na inafanya kazi vizuri, wanahabri sasa wana jukumu la moja kwa moja kuhakikisha hali inaendelea kuwa nzuri na umoja huo hauchafuliwi na vitimbakwiri, pamoja na wabinafsi ambao walikuwa wakifaidika kutokana na migogoro ya ndani iliyokuwepo baina ya Wazanzibari.
Katika kufanikisha hilo, wanahabari Zanzibar ni lazima wawe na ajenda ya kuchangia kasi ya maendeleo ya wananchi, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kukomesha siasa za chuki kwani itakuwa inayafikia matumaini ya wengi baada ya mabadiliko hayo.
Japokuwa katika ulimwengu wa maendeleo ya teknolojia ya habari kuna vyombo vya habari vikiwemo vinavyoitwa ‘new media’ kama vile simu za mkononi, bado nafasi kubwa ya kutengeneza ajenda kitaalamu inabakia kwa vyombo vya habari vya kale kama vile redio, TV na magazeti.
Tukiangalia suala la umoja wa kitaifa limeelezwa wazi katika Mkakati wa Kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar (MKUZA) kwenye Cluster 3, hivyo kwa mfumo wa serikali uliopo hivi sasa inaonekana wazi upande wa Serikali umeshatekeleza jukumu lake, kwani kuna serikali ya umoja wa kitaifa ambayo imeanza kazi vyema na kupokelewa vizuri na wananchi.
Hata hivyo, mbali ya wananchi kuupokea vyema mfumo huo na kuufurahia inaonekana bado unawachanganya au wanachanganywa na baadhi ya wanasiasa ambao hawakufurahishwa na kufanikiwa kwa juhudi za kuwepo umoja wa kitaifa Zanzibar, kwa vile maslahi yao yalitegemea kuwepo ghasia na suitafahamu, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na wanahabari kwa kuwaelimisha wananchi kwa kina.
Katika hili inashangaza kuona au kusikia baadhi ya wanahabari tena wenye kujigamba kama wanaumwa na Zanzibar, kuandika magazetini na kutangaza redioni au kuonesha kwenye TV, kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imevunja moyo matarajio ya wananchi kwa kuchambua muundo wa Serikali, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Makamishna na Wakurugenzi kwa kuzingatia U-Pemba, U-Unguja na U-CUF na U-CCM.
Uandishi wa habari kama huu kwa Zanzibar ya leo haufai kupewa nafasi kwani unakwamisha morali ya kutekeleza majukumu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa umoja wa kitaifa na badala yake unairudisha nyuma Zanzibar kwenye zama za kubaguana kwa misingi visiwa vya Unguja na Pemba na baadae tutakwenda mbele zaidi kuangalia Makunduchi, Donge, Umbuji, Fumba, Tumbatu na halafu kwenye mseto wa ushazi Mji Mkongwe.
Kuna njia nyingi ambazo Zanzibar inaweza kujikomboa na umasikini, iwapo mchango wa jamii nzima kupitia vyombo vya habari utapatikana ipasavyo, hivyo vyama vya waandishi wa habari, vyombo vya habari kimoja kimoja na waandishi wa habari mmoja mmoja, ni lazima watekeleze jukumu lao kwa kutumia uzalendo.
Aidha katika kuimarisha sekta ya habari Zanzibar, umoja na kujielimisha kwa wanahabari ni jambo ambalo litatoa mchango mkubwa katika kuendeleza ujenzi wa Zanzibar mpya na kuvifanya visiwa vya Zanzibar kuwa vyenye maendeleo endelevu, amani, umoja na utulivu wa kudumu.
Wanahabari wa Zanzibar ni lazima wajiongezee taaluma ya fani mbali mbali kila wanapopata fursa na kamwe wasiridhike na vyeti walivyonavyo sasa ambavyo vinawaweka katika mipaka ya utendaji wao kwa kutoelewa mambo mengi.
Miongoni mwa mambo yanayowapa tabu wanahabari wa Zanzibar ambayo wanapaswa kujielimisha ni pamoja na sheria za nchi, sera za kitaifa, mipango ya maendeleo ya kitaifa kama vile MKUZA na Dira ya Maendeleo ya 2020, pamoja na suala zima la katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha ni aibu lakini ukweli kwamba wanahabari wa Zanzibar wamesambaratika na kujigawa katika makundi tafauti ikiwemo Userikali na Ubinafsi, pamoja na uvyama vya siasa.
Wakati tukiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kesho, taasisi pekee inayounganisha wanahabari ambayo iko hai na inafanmya kazi kiheshima ni Klabu ya Waandishi wa Habari ya Pemba ‘Pemba Press Club’, zilizobakia kama Klabu ya Unguja na Jumuiya ya Waandishi wa habari Zanzibar (JAZ) hazina uhai.
Usishangae kuona kesho wanahabari duniani wakiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, hapa Zanzibar ikawa kimya kama vile hakuna wanahabari au vyombo vya habari ambavyo vinaathirika kwa njia moja au nyengine na dhana nzima ya uhuru wa vyombo vya habari.
Wanahabari tuelewe kwamba maadili ya uandishi wa habari yanakataza kuripoti taarifa ambayo mwandishi hana taaluma nayo na hakuifanyia utafiti wa kina.
Katika kipindi hichi ambacho Tanzania imeingia katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanahabari wengi wa Zanzibar wamekuwa wakiripoti ‘kikasuku’ kwa kukariri yanayosemwa na watu, mchango wao katikia uchambuzi wa suala hilo bado haujaonekana.
Katika suala hili iwapo vyombo vya habari vya Zanzibar havitakuwa makini vinaweza kuwa kikwazo cha mabadiliko haya, pamoja na kuachia upotoshaji wa suala hili unaofanywa na wanasiasa na vyombo vyengine vya habari dhidi ya Zanzibar kuichora kama haitaki kudumisha Muungano kilainapotoa mawazo yake.
Wanahabari nyinyi ndio mnaotegemewa na wananchi hapa Zanzibar muwaelimishe kuhusiana na mabadiliko hayo ya katiba kwa uchambuzi yakinifu ambao utazingatia misingi ya ukweli na uzalendo, huku mkijiepusha na uchochezi wa aina yoyote au kukubali kurubuniwa na vitimbakwiri.
Kuna suala zima la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo kila uchao imekuwa ikipitisha sheria na kusaini mikataba, huku wananchi wa Zanzibar wakiwa hawajui lolote hali ya kuwa nao ni wanachama wa Jumuiya hiyo na wanalazimika kutekeleza makubaliano yanayofikiwa.
Jengine muhimu ni kwa wanahabari kufanya kazi ya kuisaidia Serikali kwa kuimurika na kuonesha njia na kuikosoa pale inapokwenda kombo.
Wanahabari waelewe kwamba Serikali inafurahia kukosolewa kwani mara nyingi huwa haina taarifa za watendaji wake wakorofi, ambao wanafanya mambo kwa utashi wao kinyume na maelekezo ya Serikali, hivyo kuwafichua itakuwa msaada mkubwa kwa serikali.
Vyombo vyetu vya habari vibadilike na kuacha uandishi wa kihafidhina wa kuficha ukweli na kuvisha gamba machafu kwa kuitaja Serikali hali ya kuwa vinawaelewa wakorofi ambao hawafuati maelekezo ya Serikali.
Wanahabri ni lazima wajiheshimu ili kada yao iendelee kuheshimiwa na kuonekana kweli kama ni kiungo cha nne cha Taifa hili.
Wanahabari wa Zanzibar hivi sasa mnapaswa kutoka nje ya mipaka ya visiwa vya Unguja na Pemba, ili kuitafutia mbinu za kuiwezesha Zanzibar kufanikiwa zaidi kimaendeleo kwa kutumia taasisi mbali mbali za nje na kuwavutia wale Diaspora wa Zanzibar ambao wameenea ulimwenguni kote.
Kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano kama vile ICT, wanahabari wa Zanzibar sasa wachukue nafasi ya kuitangaza Zanzibar na fursa zilizopo.
Hali ya kisiasa Zanzibar ingekuwa ikitangazwa kiuchumi hivi sasa basi ingekuwa na nafasi kubwa kuvutia wawekezaji zaidi, pamoja na watalii ambao kwa muda mrefu wamejenga mawazo kwam,ba Zanzibar haikaliki.
Aidha si vibaya hata kuwatenga wanahabari wenzao ambao wazi wazi wanaendelea kuendekeza uchochezi dhidi ya Zanzibar na watu wake, ambao kwao mara zote habari mbay za Zanzibar ndiyo huwa habari mwanana.
Huku vyombo vya habari vikielimisha wananchi kuhusu mfumo huu mpya wa Serikali, pia vina jukumu kuwabainisha haki na wajibu wao katika kufanikisha lengo la kujenga Zanzibar mpya, yenye maendeleo endelevu, umoja, mshikamano na amani ya kudumu.
Kubwa na la muhimu kwa wananchi kueleweshwa ni kwamba mfumo huu mpya hauna maana ya kuvunjwa sheria za nchi kwa mtu kufanya atakalo, lazima sheria za nchi ziheshimiwe na kufuatwa.
Wanahabari wana nafasi muhimu katika kujenga Zanzibar mpya.
0777 471199
No comments:
Post a Comment