MUWAZA pamoja na Wazanzibari wengi ulimwenguni walisikia wito kutoka katika spitali ya Mnazi Mmoja yakwamba idara ya ICU yake haiwezi kuhudumia wagonjwa mahatuti kwa sababu ya upungufu wa vifaa maalum vilivyo vya lazima kutibu na kuokoa maisha ya wagonjwa taabani.
Kutangazwa kwa habari hizi pamoja na kwamba hali ya Zanzibar ya matibabu kwa jumla ni hairidhishi imesikitisha Wazanzibari wote pamoja wa wale tulio Ughaibuni (Diaspora).
Kwa hivyo MUWAZA ilikwenda mbio kutafuta ufumbuzi angalau wa muda, kutatua sehemu fulani ya upungufu huu.
MUWAZA ilifanya bidii ya kutafuta vifaa kadhaa vitakavyo saidia kupunguza shida zinazoikabili ICU kwa kutuma “Container” la futi 40 ambalo liko njiani kutoka Copenhagen kuendea Zanzibar.
Katika “Container” hilo lililojaa vifaa tofauti vya kusaidia ICU vimo vile vile vifaa tofauti vitakavyo saidia sehemu ya upasuaji, kama vile meza za upasuaji, gastroscope, coloscope, sigmoidoscope , bronchoscope n.k.
Orodha ya vifaa viliyomo ni ndefu na itakuwa vigumu kuvitaja vyote. Bahati mbaya nafasi ndani ya “ Container” hilo imekuwa ndogo na vifaa vingi vimebaki Copenhagen vikisubiri “Container” lifuatalo .
MUWAZA imefajirika kushirikiana na DANTAN (Danish Tanzanian Association) ya Denmark ambao walisaidia kupeleka maombi ya msaada wa fedha za kusafirishia “Container” hilo kutoka kwa Danish Volunteer NGO (MS). MUWAZA inatoa shukurani kwa DANTAN na MS kwa msaada huo.
CONTAINER HILI LINATARAJIWA KUWASILI ZANZIBAR TAREHE 20.08.2011 NA KUPOKEWA NA HOSPITALI YA MNAZI MMOJA IKISHIRIKIANA NA ZOP NA HOSPITALI YA AL-RAHMA WENYE VITU VICHACHE KATIKA MZIGO HUO.
Katika jitihada zake kuzidi kusaidia kuendeleza hali ya siha na matibabu Zanzibar, MUWAZA imefanya yafuatayo:
Tarehe 29.07.2011 ilepeleka ujumbe wa watu watatu huko Utaliana kwa madhumuni ya kupeleka madaktari Zanzibar na kusaidia katika vitengo vya magonjwa ya sehemu ya neurology sehemu ya magonjwa ya akili (psychiatry na psychology). Vile vile tunatayarishwa mpango wa kupeleka wanafunzi wa kusomea udaktari na kuwapa nafasi madaktari kwenda kufanya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Udaktari cha Rome.
Kuna mpango wa kuanzishwa kwa chuo cha wauguzi ambacho hatimae kitapandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu cha Udakitari Zanzibar.
Kundi hili la Madaktari wa Kitaliana linatarajiwa kuwasili Zanzibar kwa uchunguzi (Feasibility study) mwezi wa Februari, 2012, wakiwa ni wageni wa Serikali ( Wizara Ya Afya na Ustawi wa Jamii).
MUWAZA vile vile ilifanya mazungumzo na kukubaliana na madaktari wa macho ambao wanatarajiwa kufika Zanzibar mnamo mwezi wa Septemba/Disemba 2011 kwa uchunguzi. Ni matarajio yetu serikali itawapokea vizuri.
MUWAZA inachukua juhudi ya kuwatafuta, kuwakusanya madaktari wa Kizanzibari walio nje ili kutayarisha Kongamano lenye lengo la kuinua maendeleo ya Afya Zanzibar. Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika London.
Katika juhudi zake kuleta maendeleo Zanzibar MUWAZA inakusudia kushirikiana na Zanzibar Outreach Programme (ZOP), Outreach Zanzibar Foundation ya Canada, ZAWA, Zanzibar Diaspora ya Skandinavia pamoja na kukaribisha Diaspora nyengine za Kizanzibari kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni.
Mwezi wa Oktoba MUWAZA itapeleka ujumbe huko Ufaransa kuhudhuria “Trade Fair” ambayo itajumuisha kati ya mambo mengine uvuvi wa Bahari Kuu. Tunatarajia kupata mjumbe kutoka wizara hiyo huko Zanzibar.
Dr. Yussuf S. Salim
Mwenyekiti wa MUWAZA
Copenhagen
Denmark
No comments:
Post a Comment