Habari za Punde

JAPAN KUENDELEA KUIUNGA MKONO ZANZIBAR


Na Rajab  Mkasaba

JAPAN imeeleza azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na kutoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein na wananchi wa Zanzibar kufuatia kuzama kwa meli ya MV Spice Islander hivi karibuni.


Balozi wa Japan anaemaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania, Mhe. Hiroshi Nakagawa aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Dk. Shein ikiwa ni pamoja na kuja kuaga.

Katika maelezo yake, Balozi nakagawa alieleza kuwa Japan inajivunia uhusiano mkubwa uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa nchi yake itaimarisha na kukuza zaidi uhusiano huo.

Alisema kuwa Japan itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuendeleza sekta ya kilimo kupitia mradi wake mkubwa wa JICA.

Balozi Nakagawa alisema kuwa mbali ya mradi huo Japan imekuwa ikiendesha miradi mbali mbali mikubwa ukiwemo mradi wa Maji na kueleza kuwa nchi yake itaendelea kutoa msaada wake katika kuhakikisha mradi huo unapata mafanikio makubwa kama ilivyotarajiwa.

Katika maelezo yake Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa Japan itaendeleza miradi yake iliopo na kuiimarisha zaidi ili iweze kuleta mafanikio.

Aidha, Balozi wa Japan alimpa mkono wa pole Dk. Shein kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar kufuatia msiba mkubwa uliotokea hivi karibuni wa kuzama kwa meli ya MV Spice Islendar na kusababisha vifo na majehudi kadhaa.

Pamoja na hayo, Balozi huyo wa Japan alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake bado ina nia ya kusaidia ujenzi wa bandari ya wavuvi huko Malindi mjini Unguja, hatua ambayo pia, itasidia kuimarisha sekta ya uvuvi hapa Zanzibar.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na mashirikiano yaliopo kati yake na Japan.

Dk. Shein alisema kuwa kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla anapokea mkono wa pole kufuatia msiba mkubwa wa kuzama kwa Meli ya Spice Islandar uliotokea hivi karibuni hapa nchini.

Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa shukurani na pongezi kwa Serikali ya Japan kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Dk. Shein alimueleza Balozi Nakagawa kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Japan, na kuahidi kuwa Zanzibar itauimarisha zaidi.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa tayari Zanzibar imejiwekea mazingira mazuri ya uwekezaji hasa katika sekta ya uvuvi na kuishauri Japan kuekeza katika sekta hiyo.

Dk. Shein pia, alimumueleza Balozi huyo kuwa katika sekta ya Utalii, juhudi mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa na serikali ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika hivyo, katika mazungumzo hayo alitaka watalii kutoka Japan kuja kuitembelea Zanzibar.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa Japan kwa kuendela kuisaidia na kutoa mashirikiano yake na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu, kilimo na nyenginezo. Pia, Dk. Shein alitoa pongezi Japan, kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar kwa kupata Waziri Mkuu mpya Mhe. Yoshihiko Noda aliechaguliwa hivi karibuni.

Wakati huo huo, Ujerumani imeeleza kusikitishwa na tukio la kuzama kwa meli ya MV Spice Islande na kumpa mkono wa pole Rais Dk. Shein kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar huku ikiahidi kukuza uhusiano sambamba na kuendelea kusaidia miradi ya maendeleo.

Balozi wa Shirikisho la Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Klaus-Peter Brandes aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofika kwa ajili ya kujitambulisha na kueleza kuwa mikakati kabambe imewekwa na nchi yake katika kuimarisha zaidi miradi ya maendeleo kati ya mwaka 2012 hadi 2013 hapa nchini.

Aidha, Balozi huyo wa Ujerumani aliimpongeza Zanzibar kwa kupata mafanikio makubwa kisiasa na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuendela kupata maendeleo endelevu.

Nae Dk. Shein aliipongeza Ujenrumani kwa kuiunga mkono Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya afyam elimu na nyengine na kusisitiza kuwa juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuimarisha demokrasia hapa nchini hatua ambayo inaendelea kuipa sifa kubwa Zanzibar kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.