Habari za Punde

MASOUD AFUATA NYAYO ZA MSOMA

Na Haji Nassor, Pemba

SIKU chache baada ya Kamati Tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuthibitisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa na Usuluhishi Abdulghan Msoma, Makamu Mwenyekiti wake Amran Masoud naye ametangaza rasmi kubwaga manyanga.

Katika barua yake ya Disemba 28, mwaka huu, Masoud ametaja sababu za kuchukua uamuzi huo, kuwa ni kukabiliwa na majukumu mazito ya kikazi yanayohitaji muda wa kutosha na umakini mkubwa.


"Pamoja na heshima mliyonipa ZFA Taifa kwa kunichagua kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa na Usuluhishi, lakini naomba mniruhusu kuiacha nafasi hiyo kwa vile nimezidiwa na majukumu ya kazi
yanayohitaji umakini mkubwa", ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Nakala ya barua hiyo iliyopelekwa kwa Katibu Mtendaji wa ZFA Taifa ambayo Zanzibar Leo inayo nakala yake, imefafanua kuwa, kutokana na mazingira ya kazi yanayomkabili, anaamini hataweza kutekeleza ipasavyo majukumu ndani ya Kamati hiyo kwa ufanisi unaotarajiwa.

Amran Masoud ambaye pia ni Ofisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Pemba, aliteuliwa kukalia kiti hicho mwaka jana.

Baada ya Msoma kuachia ngazi kwa sababu za kiafya, ZFA ilimchagua Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mjini Mkadam Khamis Mkadam kuwa Mwenyekiti mpya, na tayari amethibitishwa na Kamati Tendaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.