Habari za Punde

Judo TZ kushindana Morocco

Watakaopata medali kushiriki Olimpiki London

Na Mwandishi Wetu

WACHEZAJI judo sita wa timu ya Taifa ya Tanzania, wanatarajiwa kwenda nchini Morocco kushiriki mashindano ya 33 ya bara la Afrika ya mchezo huo, yaliyopangwa kuanza Aprili 1 hadi 6, mwaka huu.

Wanajudo watakaotwaa medali za dhahabu, fedha na shaba katika mashindano hayo, ndio watakaoiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki inayotajiwa kufanyika jijini London Uingereza mwezi Juni mwaka huu.

Wachezaji wanne kati ya hao pamoja na kocha mmoja, wanagharamiwa safari yao na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), huku Jeshi la Magereza likiwagharamia wachezaji wawili ambao ni waajiriwa wake.

Hao ni miongoni mwa wachezaji wanane waliokuwa wamepiga kambi katika ukumbi wa judo ‘Budokan’ uliopo uwanja wa Amaan mjini hapa.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Tsuyoshi Shimaoka amefahamisha kuwa, wachezaji hao wamekuwa katika mazoezi makali yaliyoanza tarehe 7 hadi 28 Machi, mwaka huu kujiandaa kwa ajili ya patashika hiyo ya Morocco.

Shimaoka ambaye pia ni Rais wa Chama cha Judo Zanzibar (ZJA), amewataja wanajudo hao na uzito wao ukiwa katika mabano, kuwa ni Azzan Hussein Khamis (U-60), Abdulsamad Alawi Abdallah (U-73) na Mohammed Khamis Juma (U-81) wote kutoka Zanzibar.

Mwengine ambaye ametokea Tanzania Bara ni Andrea Thomas Mlugu (U-66), pamoja na wale wa Magereza ambao ni Gervas Leonard Chilipweli (U-81) pamoja na Geophrey Edward Mtawa (U-100).

Tshimaoka amesema wachezaji wote hao wako katika hali nzuri na ari ya hali ya juu, na kwamba anatumai kuwa watafanya vyema ili kuipeperusha vizuri bendera ya Tanzania na hatimaye kukata tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki.

Wachezaji wa timu hiyo wanatarajiwa kuondoka nchini kesho asubuhi kwa ndege ya Shirika la Egypt Air, kwenda Morocco tayari kusaka medali na tiketi za michezo ya Olimpiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.