Habari za Punde

Mashua za KMKM zazama Kikwajuni

Na Ali Cheupe

MABAHARIA wa KMKM juzi walizamishwa na mabondia wenzao timu ya Kikwajuni kwa kichapo cha mabao 5-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Zanzibar, uliopigwa uwanja wa Mao Dzedong.

Timu zote zililazimika kucheza bila wachezaji wake kadhaa tegemeo kutokana na kufungiwa kwa kitendo cha kupiga waamuzi katika michezo tafauti ya ligi hiyo.

Kikwajuni iliwakosa wanandinga tisa waliotiwa korokoroni kwa kumtwanga mwamuzi Waziri Sheha siku ilipocheza na Zimamoto, huku KMKM ikicheza bila nyota wake watano kwa utovu wa nidhamu kama huo wa kumuangushia kisago mwamuzi Hassan Gerei kwenye uwanja wa Gombani ilipokutana na Super Falcon.

Katika mchezo huo Kikwajuni ilikuwa ya kwanza kuzifumania nyavu kwa bao la dakika ya pili lililowekwa kimiani na Bakari Thani baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na mlinda mlango wa KMKM.

Mchezaji huyo pia alifunga goli la pili na la nne mnamo dakika za 47 na 75 mtawalia, huku mengine yakifungwa na Ramadhan Hussein kwenye dakika ya 62 na 79.

Wanamaji wa Kibweni walijipatia magoli yao kupitia kwa mchezaji Hashim Ramadhan katika dakika ya 43 na Said Khalid aliyecheka na nyavu katika dakika ya 59.

Katika pambano hilo hakukosekana vituko, ambapo Kikwajuni ilicheza ikiwa pungufu ya mmchezaji mmja kwa muda wa dakika saba baada ya mchezaji Rashid Mohammed kuumia kwenye dakika ya 18, lakini hakukuwa na mchezaji hata mmoja wa akiba katika benchi.

Mchezaji Majid Mohammed aliyeingia kuchukua nafasi yake aliwasili uwanjani bila jezi akitokea nyumbani na kuingia uwanjani katika dakika ya 25 baada ya kubadili nguo.

Aidha mwamuzi wa pambano hilo Ali Omar 'Kisaka' alilazimika kumfurusha katika benchi la ufundi mfadhili wa Kikwajuni Jaku Hashim aliyekuwa akilalamikia maamuzi yake, ambaye hata hivyo hakuendelea kubaki majukwaani na kuondoka zake.

Kufuatia matukio kadhaa ya vurugu na kupigwa na waamuzi, askari jeshi la Polisi walionekana kwa idadi kubwa baada ya kukatisha kwa wiki kadhaa desturi ya kuwepo uwanjani hapo.

Kwa matokeo hayo, timu ya Kikwajuni imefikishga pointi 15 kutokana na michezo 15 pia, ikichupa hadi nafasi ya tisa kutoka ya 11 na kuishusha Polisi yenye pointi kma hizo kwenye nafasi ya kumi, ikiwa imeshuka dimbani mara 16.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.