Habari za Punde

Cossovo mambo safi

Haji Nassor, Pemba

TIMU ya Cossovo ya Chumbageni Wambaa, imefanikiwa kusonga mbele hatua ya nane bora, kwenye ligi daraja la pili Wilaya ya Mkoani, baada ya kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 19.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Marzouk Mabrouk, amesema hatua waliyofikia walikuwa na uhakika nayo kutokana na kuziangusha timu kadhaa walizokuwa wakikumbana nazo.

Amesema baada ya kufanikiwa hatua hiyo, kwa sasa wameongeza muda wa mazoezi na kushuka dimbani mara mbili kila siku kwa mazoezi makali.

Aidha, alisema iwapo Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mkoani kitatoa nafasi ya kusajili wachezaji zaidi, wanatarajia kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji na ulinzi ili kujiimarisha kabla kuanza kwa hatua hiyo ya nane bora.

Timu nyengine zilizofanikiwa kutinga hatua hiyo ni Muungano, Charanga na Pindua.

Timu hiyo iliyoasisiwa misimu miwili iliyopita, imefanikiwa kupanda daraja la pili msimu uliomalizika na imetinga hatua ya nane bora na kuziacha timu za Aston Villa na Maendeleo ambazo pia zina maskani yao Chumbageni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.