Habari za Punde

Super Falcon Yachanua kileleni

Miembeni, Mundu ngoma nzito

Na Salum Vuai, Maelezo

WAKATI Ligi Kuu ya soka Zanzibar ikienda likizoni kwa siku 12, timu iliyopanda daraja msimu huu Super Falcon, ndiyo inayoongoza katika msimamo ikiwa imefikisha pointi 29 baada ya kushuka dimbani mara 16.

Timu hiyo ambayo ilianza ligi kwa kusuasua, imeweza kuwashangaza wengi kwa kuzinduka na kuzibeba timu nyengine 11 zinazoshiriki ngarambe hizo, wakiwemo mabingwa watetezi Mafunzo.

Nafasi ya pili inashikiliwa na timu ya Jamhuri iliyoiwakilisha Zanzibar kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo imetia mkononi pointi 28, kutokana na michezo 16 iliyocheza, huku Miembeni United ambayo pia imecheza mechi 16 ikiwa na akiba ya pointi 25 iko katika nafasi ya tatu.

Mabingwa wa msimu uliopita Mafunzo, Chipukizi na KMKM zote zimejikusanyia pointi 24 kila moja zikiwa katika nafasi ya nne, tano na sita mtawalia zikipishana kwa tafauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo, Mafunzo imecheza mechi chache, 14, ikilinganishwa na timu nyengine hivyo inaweza kupanda ikiwa itafanya vizuri katika mechi zake za viporo zinazotarajiwa kuchezwa kabla ligi hiyo kurudi dimbani.

Wakati timu za Zimamoto yenye pointi 23 na Chuoni pointi 18 kutokana na mechi 16, zikiwa katika nafasi za katikati mambo yanaonekana kuwa mazito kwa wakongwe Miembeni SC na Mundu, ambazo zote zinakabiliwa na hatari ya kuteremka daraja, kama hazitaamka mapema na kupigana kwa nguvu kuepuka balaa hilo.

Miembeni yenye historia kubwa katika soka la Zanzibar, Tanzania na Afrika Mashariki, bado inasoka katika nafasi ya pili kutoka mkiani, ikiwa na akiba ya pointi 13, juu ya wavuvi wa nguru kutoka Nungwi, timu ya Mundu, ikiburura mkia wa ligi hiyo na akiba ya pointi 10, ikiwa timu pekee iliyocheza mechi nyingi, 17, kuliko zote zinazoshiriki ligi hiyo.

Mabingwa mara kadhaa, Polisi iko katika nafasi ya kumi kwa kukusanya pointi 15 ikiwa imecheza mechi 16, sawa na Kikwajuni ambayo imeshuika uwanjani mara 15.

Ligi hiyo inatarajiwa kurudi tena viwanjani Aprili 11, mwaka huu ambapo ratiba mpya inaandaliwa na Kamati ya Ligi iliyoko chini ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.