Na Haji Nassor, Pemba
TIMU ya usimamizi wa mradi wa utambuzi na usajili wa ardhi Zanzibar, imesema itawabana wamiliki wa ardhi ambao sio wazanzibari kwa kukodishwa na sio kupatiwa hati za umikili sawa na wazawa.
Timu hiyo ilisema wakati Zanzibar ikiwa katika katika mchakato wa utambuzi na hatimae usajili wa ardhi, kwa mujibu wa sheria hiyo wasiokuwa wazanzibari hata kama waliuziwa maeneo hayo, watakodishwa.
Mwenyekiti wa Timu hiyo ambae pia ni Mkurugenzi wa Ardhi Zanzibar Januari Fusi, alisema hayo jana huko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba wakati timu hiyo ilipojitambulisha na kueleza namna mchakato wa utambuzi na usajili wa ardhi ulivyo.
Fusi alisema zoezi hilo linalenga zaidi wazanzibari (wazalendo), hivyo iwapo kuna mgeni na anamiliki ardhi, serikali itamkodisha na sio kumpatia hati ya umiliki kama walivyo wazaliwa.
“Hilo ni changamoto kubwa ambayo huwenda ikajitokeza wakati zoezi litakapokuwa linaendelea, lakini sheria hii imewaka wazi ni nani anapaswa kumilikishwa ardhi baada ya kuisajili”, alisema Fusi.
Aidha alisema kuwa hata kuna mtu tayari ameshamiliki ardhi na anaowaraka kamili kwa mujibu sheria za umiliki, nae atapswa kufanyiwa uhakiki na kisha kusajiliwa ardhi yake.
Mwenyekiti huyo alifafanua lengo hasa la zoezi hilo, ni kuepusha migogoro ya ardhi ambayo kwa sasa hapa Zanzibar imeshamiri na yakichangiwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na eneo moja kumilikiwa na zaidi ya watu wawili.
Aliongeza kuwa anaamini zoezi hilo ambalo litakua shehia moja baada ya nyengine, litakua na mafanikio makubwa hasa kwa vile awali wananchi husika wataelimishwa hadi wafahamu kisha zoezi hilo kufanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, alisema wasiwasi wake ni kwa mahakimu ambao wakati mwengine hukiuka sheria kwa kula rushwa na kumpa haki mtu asiyestahiki.
“Katika hili la usajili watatokezea wanyonge waende mahakamani kudai haki zao, lakini je sheria na taratibu za usajili wa ardhi zitamlinda vipi mnyonge’’,alihoji Mkuu huyo wa Mkoa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Jabu Khamis Mbwana, alisema hilo linaweza kufanikiwa iwapo ushirikiano utaendelea miongoni mwa maofisa wa tume hiyo na wananchi pamoja na makundi mengine.
Hata hivyo alisema suala la kuwashirikisha wananchi wa shehia husika ni vyema likapewa kipaumbele ili liweze kufanikiwa vyema.
Kwa upande wa wilaya ya Mkoani shehia ambayo itaanza kama majaribio ni shehia ya Chokocho ambapo tayari shehia ya Kiungoni kwa wilaya ya Wete iko katika hatu nzuri baada ya kuanza kwa zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment