Na Khadija Khamis, Maelezo Zanzibar
WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Áfrika ( ADB) kwa kuendeleza mradi wa elimu mbadala na amali kwa awamu ya pili.
Akitoa shukrani hizo leo huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Zanzíbar wakati akizindua mradi huo wa awamu ya pili ambao umelenga kupunguza umasikini miongoni mwa watoto na vijana ambao hawakuweza kumaliza masomo yao ya skuli na wale ambao hawakubahatika kupata elimu kabisa.
Jumla ya dola za kimarekani milioni 23 zimetolewa na Benki hiyo kwa ajili ya kuendeleza mradi wa elimu mbadala na amali.
Waziri huyo alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuwapa uwezo vijana wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na kuwapatia mafunzo mbali mbali ya ujuzi ambao utawasaidia kimaisha.
Aidha alieleza kuwa pamoja na juhudi hizo za wafadhili kazi iliyopo hivi sasa ni kutoa mashirikiano ya pamoja kwa wale wadau wa kubwa wa Wizara tatu tofauti
Akizitaja Wizara hizo ambazo ni wadau wa elimu mjumuisho ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika.
“Kazi iliyokuwepo mbele yetu ni kubwa sana anahitaji mashirikiano kwa umoja wetu” alisema Haroun.
Alisema kuwa juhudi na maarifa ya pamoja yanauwezo wa kuliondoa suala la umasikini kwa vijana kwani nchi nyingi zimeweza kujikwamua na umaskini kutokana na kazi za amali
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, alisema kuwa kuwapa mafunzo ya ufundi wanafunzi hao kutachangia kiasi kikubwa kupata ajira Serikalini au kujiajiri wenyewe kutokana na ujuzi wao.
Pia alisema kuwa anaahidi mradi huo utakuwa ni mradi endelevu ambao utaweza kuzalisha fedha nyingi kutokana na vituo vya kazi ya amali mbali mbali vitakavyoanzishwa pamoja na kuingizwa chuo cha utalii katika mradi huo.
“Programu ya utalii kwa wote mafanikio ya awamu ya pili yataengeza kutoa ujuzi kupitia shughuli za kitalii ”alisema Shamuhuna.
Sambamba na hayo nae Mwakilishi Mkaazi wa (ADB) Tom Kandiero alitoa shukrani zake za dhabi kwa kuweza kutekeleza kwa vitendo kwa mkataba wa awamu wa kwanza na kuwamini kwamba na mradi wa awamu ya pili utatekelezwa vizuri.
Mradi huo wa elimu mbadala na amali wa awamu ya pili umezinduliwa rasmi leo na waziri wa kazi uwezeshaji uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Áfrika na mradi huo huo wa awamu ya kwanza ulizinduliwa 2001.
No comments:
Post a Comment